JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kuna rai tofauti za Maulamaa kuhusu mas-ala haya; kuna waliosema kwamba mwanamke aliyetoka kwenye janaba kisha akapata hedhi hana haja ya kuoga ghuslu ya janaba kwa sababu hali yake itakuwa hajatwahirika, hivyo atakapomaliza hedhi atafanya ghuslu kwa nia mbili ya kuondosha janaba na kuondosha hedhi. Ama rai nyingine na ambayo ndiyo bora zaidi na yenye usahihi zaidi , na Allaah Anajua zaidi, ni kwamba mwanamke anapotoka kwenye janaba kisha akapata hedhi afanye ghuslu ya janaba kwanza kisha atakapomaliza hedhi afanye ghuslu ya hedhi. Rai hii zaidi ni ya Maulamaa waliotoa hukumu kwamba mwenye janaba hawezi kusoma Qur-aan, bali mwenye hedhi anaweza kusoma, hivyo kufanya ghuslu kuondoa janaba kutamruhusu mwanamke kupata fursa ya kusoma Qur-aan. Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema katika Al-Mughniy (1/134): "Mwanamke akifanya ghuslu ya janaba wakati amepata hedhi, ghuslu yake itafaa na atatoka katika hukmu ya janaba" Hii ni rai ya Imaam Ahmad pia ambaye amesema: "Mwanamke atatwaharika na Janaba lakini atakuwa bado hajatwaharika na hedhi hadi damu isite". Akasema: "Simjui yeyote aliyesema kwamba mwanamke haimpasi kufanya ghuslu isipokuwa 'Atwaa, hata hivyo imesimuliwa kuwa amesema mwanamke afanye ghuslu" Kwa hiyo ni bora mwanamke aliyefikwa na hali hiyo afanye ghuslu ya janaba kwanza ili kujitoa katika hali hiyo. Na Allaah Anajua zaidi
Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
Ghuslu - Vipi Kukoga Janabah, Nifaas Na Hedhi