Anaweza Kuswali Ikiwa Atatokwa Na Manii Bila Ya Kitendo Cha Ndoa?

Je, mtu akishikana na mkewe mpaka akatoka manii bila ya kufanya tendo la ndoa anaweza kusali bila ya kuoga janaba?.

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah. Janaba inapatikana kwa hali ya kutokwa na manii sawa ikiwa manii yamekutoka kwa kuingiliana (yaani kwa kuzama kichwa cha dhakari ndani ya utupu wa mwanamke) au kuota, au kujichua n.k., na kwa hali hiyo huwezi ukaswali mpaka ujitwaharishe. Anasema Allaah "Enyi mlioamini msiikaribie Swalah, hali mkiwa mmelewa mpaka myajuwe mnayoyasema, wala hali mkiwa na janaba- isipokuwa mmo safarini mpaka mkoge" (An-Nasaaiy: 43) Na katika Sunnah anasema Ummul-Muuminiyna ‘Aaishah (radhiya Allahu 'anha) kuna Mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayemjamii mke wake kisha akakatisha ile jimai (katikati bila ya kushusha manii): Je, analazimika kuoga (janaba)? Na Bi ‘Aaishah wakati huo akiwa ameketi - Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Kwa hakika mimi na huyu bibie hufanya hivyo kisha tunakoga" (Muslim) Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi ya maudhui hiyo: Ikiwa Mtachezeana Tu Na Kutokwa Manii Inapasa Kukoga Josho? Je, Inapasa Kufanya Ghuslu Baada Ya Kutokwa Na Manii Bila Ya Kujimai? Na Allaah Anajua zaidi
Vitambulisho: