Akiwa Ameshaoga Kisha ukapita Muda Inabidi Atawadhe ili Kuswali?

SWALI: Je waweza toka kuoga vizuri mtu kwako na wakati wa swala umewadia ukaswali bila kutawadha ikiwa una uhakika upo safi japo nyumbani? Natumai waislam wenzangu mmenielewa kidogo nategemea mafanikio kwenu ya kielimu kubwa msinisahau mie ni mwenzenu.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuoga na kupita kwa muda baada ya hapo. Hakika ni kuwa kuoga na kutawadha ni vitu viwili tofauti. Kuoga ni kujiosha mwili mzima kwa utaratibu unaotaka wewe ilhali kutawadha ni kuosha viungo fulani kwa utaratibu ulioelezewa na Allaah Aliyetukuka katika Qur-aan na Mtume Wake mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hata hivyo kila jambo ni kwa Niyah, ikiwa umeweka Niyah kuwa kuoga kwako huko kutajumuisha na twahara ya Hadathi ndogo kwa kuwakilisha Wudhuu, basi kuoga kwako kutakuwa kunatosheleza na utaweza kuswali baada ya kuoga kwako. Kadhalika kuchukua Wudhuu ni jambo bora zaidi na mja hupata ujira kwa kutawadha au kuufanya upya Wudhuu wake. Ama aliyeoga josho la kishari’ah na akataka kuswali, basi si lazima atawadhe hata kama alikuwa hajatawadha wakati akioga, kwani twaharisho la janaba linaondosha vile vile twaharisho la hadathi ndogo (kutokuwa na wudhuu). Hii ni kwa vile vizuizi vya janaba ni vingi zaidi kuliko vizuizi vya hadathi ndogo. Hivyo basi, kidogo humezwa na kingi. Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akisema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa hatawadhi baada ya kuoga janaba”. Hadiyth Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah. Na katika riwaya nyingine: “Anaoga na anaswali rakaa mbili, na wala simwoni akifanya wudhuu baada ya kuoga.” Hadiyth Sahihi kwa nyingine: Imetolewa na Abuu Daawuud na Ahmad Na Allaah Anajua zaidi
Vitambulisho: