Kutayamamu

12562

 

Maana ya Kutayamamu

Kutayamamu kilugha

Kukikusudia kitu na kukielekea

Kutayamamu kisheria

Kupukusa uso na mikono miwili kwa ardhi twahara kwa nia ya kujitwahirisha

Hukumu ya kutayamamu

Inapasa kutayamamu yakikosekana maji au ikawa haiwezikani kuyatumia kwa jambo linalolazimu utwahara kama vile Swala. na kutayamamu kunapendekezwa katika kufanya jambo linalopendekezwa kama vile kusoma Qur›ani.

Dalili za kutayamamu kisheria

1. Mwenyezi Mungu U Anasema: {Mkitopata maji kusudieni ardhi nzuri, mpanguse nyuso zenu na mikono yenu kwa hiyo} [5: 6]

2. Amesema Mtume ﷺ: (Nimepewa mambo matano hakuna aliyepewa kabla yangu: Nimenusuriwa kwa kitisho masafa ya mwezi, nimefanyiwa ardhi kuwa ni mahali pa kuswali na pa kujitwahirishia: kwani yoyote katika umma wangu atakayeingiliwa na kipindi cha Swala na aswali) [ Imepokewa na Bukhari.].

Hekima ya Sheria kuweka kutayamamu

1. Kuwasahilishia umma wa Mtume Muhammad ﷺ

2. Kuepusha madhara yanayosababishwa na utumiaji maji katika hali ya ugonjwa, na baridi kali na mfano wa hayo.

3. Kudumisha mafungamano ya ibada yasikatike kwa kukosekana maji, au kutoweza kuyatumia

Niwakati gani mtu anafaa kutayamamu

1. Yanapokosekana maji

Kwa neno lake Mwenyezi Mungu aliyetukuka: {Na mkitopata maji tayamamuni} [5: 6].

Na mtu haambiwi kuwa amekosa maji iwapo hakuyatafuta.

2. kushindwa kuyatumia maji

Kama mgonjwa au mkongwe asiyeweza kutembea, na akawa hana wa kumsaidia kutawadha.

Mgonjwa
Mtu mzima

3. Wakati wa kuchelea madhara kwa kutumia maji

Miongoni mwa hayo:

a. Mgonjwa ambaye angeyatumia maji ugonjwa wake utazidi.

b. Mtu aliye mahali penye baridi kali na asiwe na kitu cha kupasha maji moto na akawa na yakini lau ataoga atapatikana na ugonjwa. Hii ni kwa hadithi iliyothubutu kuwa Mtume ﷺ alimkubalia ‘Amr bin al-’Asw alipowaswalisha wenzake hali akiwa ametayamamu kwa sababu ya baridi kali [ Imepokewa na Abu Daud.].

c. Awapo mahali mbali na hana maji isipokuwa kidogo ambayo anayahitajia kwa kunywa na hawezi kuleta mengine.

Namna ya kutayamamu

1. Aupige mchanga kwa mikono yake pigo moja.

2. Kisha aipulize kupunguza vumbi.

3. Kisha apanguse uso wake kwa hiyo mikono mara moja.

4. Kisha apanguse upande wa nje wa wa vitanga vya mikono. Apanguse sehemu ya nje ya kitanga cha mkono wa kulia kwa sehemu ya ndani ya kitanga cha mkono wa kushoto, kisha nje ya kitanga cha mkono wa kushoto kwa sehemu ya

Na dalili ya namna ya kutayamamu ni hadithi ya Ammar t kwamba Mtume ﷺ alipiga ardhi kwa vitanga vyake viwili vya mkono, akavipuliza kisha akapangusa uso wake na vitanga vyake kwavyo) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Kupiga mchanga kwa mikono miwili
Kupuliza mikono miwili
Kupangusa uso
Kupangusa mkono wa kulia kwa wa kushoto
Kupangusa mkono wa kushoto kwa wa kulia

Faradhi za kutayamamu

1. Kutia nia.

2. Kupangusa uso.

3. Kupangusa vitanga vya mikono.

4. Kufuatanisha: aanze kupangusa uso kisha vitanga viwili vya mikono.

5. Kufuliliza: Apanguse mikono miwili baada ya kupangusa uso papo kwa papo.

Vitanguo vya kutayamamu

1. pakipatikana maji.

2. kutukiwa mojawapo ya vitanguo vya udhu.

3. Kutukiwa na chenye kupasisha kuoga kama kuota.

4. Kuondokewa na udhuru wa kutayamamu uliowekwa na Sheria, kama ugonjwa na mfano wake.

pakipatikana maji
Imethubutu Kielimu
Kwamba mchanga wa ardhi unakusanya kwenye chembechembe zake mada ya kutakasa. Mada hii inaweza kumaliza aina zote za vijidudu, na inaweza kumaliza virusi.

Maelezo

1. Kuswali kwa kutayamamu, iwapo haiwezekani kutumia maji, ni bora kuliko mtu kuswali na huku amejizuia mkojo au choo.

2. Inafaa kutayamamu kwenye ukuta au mswala na mfano wa hivyo, iwapo kuna mchanga au vumbi juu yake.

3. Yafaa kwa mwenye kutayamamu kuswali, kwa tayamamu moja, swala atakazo za faradhi na za sunna, iwapo bado hajatangukwa na tayamumu yake.

4. Yafaa kwa mwenye kutawadha kumfuata mwenye kutayamamu, kwa kuwa Mtume ﷺ alimkubalia ‘Amr bin al-’Asw t alipowaswalisha wenzake hali ya kuwa ametayamamu kwa ajili ya baridi kali [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

5. Mwenye kutayamamu na akaswali, kisha akapata maji kabla ya wakati kutoka, hatairudia ile swala. Abu Said al-Khudri t amepokewa akisema: (Walitoka watu wawili safarini, wakati wa Swala ukaingia na wao hawana maji, wakakusudia ardhi nzuri wakatayamamu na wakaswli, kisha wakapata maji ndani ya wakati, mmoja wao akarudia swala na udhu, na yule mwingine asirudie. Kisha wakamjia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ wakamuelza hayo, akasema kumwambia yule ambaye hakurudia “Umepata Sunna na Swala yako imekutosheleza” na akmwambia yule aliyetawadha na akarudia “Wewe una thawabu mara mbili”) [ Imepokewa na Abu Daud.].

6. Mwenye kutayamamu kisha akapata maji kabla ya kuswali au katikati ya Swala, itamlazimu kujitwahirisha kwa maji, kwa kauli ya Mtume ﷺ: (Hakika ardhi nzuri ni twahirisho kwa Muislamu, hata kama hatapata maji miaka kumi. Atakapopata maji basi ayatumie kwenye ngozi yake ya mwili, kwani hilo ni kheri) [ Imwpokewa na Tirmidhi].

7. Hakuna cha kumfunga Muislamu na Swala wala kuichelewesha wakati wake. Akitoweza kutumia maji au asipoyapata, atatayamamu, akielemewa na kutayamamu pia, basi ataswali bila twahara.

8. Mwenye kukosa vitwahirisho viwili (maji na mchanga) ataswali wakati ukiingia bila ya twahara wala haimlazimu kurudia, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amesema: {Mcheni Mwenyezi Mungu mnavyoweza} [64: 16].