Swala ya wenye nyudhuru (wasiojiweza)

12172

Maelezo kuhusu Nyudhuru

Nyudhuru

Ugonjwa, Safari na Hofu

1. Swala ya mgonjwa

Inamlazimu mngonjwa kutekeleza Swala kwa kadiri ya uwezo wake. Akiwa ataweza kuilipa kama mwenye afya itamlazimu afanye hivyo. Na akiwa hawezi, basi ataitekeleza kulingana na uwezo wake.

Mgonjwa anapaswa aswali kwa kusimama akiwa anaweza kusimama. Akiwa hawezi kusimama, basi ataswali kwa kukaa. Akitoweza kukaa, ataswali kwa ubavu na uso wake uwe umeelekea Kibla. Akitoweza kuswali kwa ubavu wake, ataswali kwa kulala kwa mgongo, na miguu yake iwe imeelekea kibla iwapo hilo ni sahali kwake, akitoweza kufanya hivyo basi ataswali kulingana na hali yake ilivyo.

Na dalili ya hayo yaliyotangulia ni neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: {Muogopeni Mwenyezi Mungu vile mnvyoweza} [64: 16].

Na neno lake Mtume ﷺ kumwambia ‘Imraan bin Huswain t: (Swali kwa kusimama. Ukitoweza swali kwa kukaa. Na ukitoweza, swali kwa ubavu) [Imepokewa na Bukhari.].

Miongoni mwa hukumu za Swala ya mngonjwa

1. Mgonjwa akiswali kwa kukaa na akawa anaweza kusujudu, itamlazimu kusujudu.

2. Akiswali kwa kukaa na asiweze kusujudu, basi ataashiria kwa mwili wake kwa kurukuu na kusujudu, na sijida yake iwe chini zaidi kuliko rukuu yake. Iwapo ni uzito kwake yeye kuashiria kwa mwili wake, basi ataashiria kwa kichwa chake.

3. Iwapo ni tabu kwa mngonjwa kujitwahirisha kwa kila Swala, au ikawa ni shida kuziswali Swala katika nyakati zake, basi inafaa akusanye baina ya Swala ya Adhuhuri na ya Alasiri, na baina ya Swala ya Magharibi na ya Isha katika wakati wa Swala ya kwanza au ya pili, kulingana na lile analoliona kuwa sahali zaidi kwake.

4. Mgonjwa harusiwi kuacha Swala kabisa madamu ana akili yake. Haifai kwa mngonjwa kudharau Swala, kwa hoja kuwa yeye ni mngonjwa, na ajitahidi awezavyo kutekeleza Swala.

5. Iwapo mgonjwa anakosa fahamu kwa siku kadha kisha anazinduka, ataswali anapozundukana kulingana na uwezo wake. Na haitamlazimu kuzilipa swala zilizompita akiwa hana fahamu. Lakini iwapo kukosa fahamu kwake ni kuchache kama vile siku moja au mbili – kwa mfano-, basi itamlazimu kulipa popote an anapopata nafasi kufanya hivyo.

Kurukuu
Kusujudu
Kupiga Takbiri
Kisomo

2. Swalah ya msafiri

Msafiri ameruhusiwa na Sheria kupunguza Swala za rakaa nne-nne (Adhuhuri, Alasiri na isha) kuzifanya rakaa mbili-mbili, pia kukusanya Swala ya Adhuhuri pamoja na Alasiri na ya Magharibi pamoja na Isha, kwa neno la Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka: {Na mkisafiri kwenye safari, si makosa kwenu nyinyi kufupisha Swala, mkiogopa kufitiniwa na makafiri, kwani makafiri kwenu nyinyi ni maadui walio wazi} [4: 101]

Na kwa hadithi iliyothubutu kutoka kwa Anas bin Malik t kwamba alisema: (Tulitoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kutoka Madina hadi Makka, na akawa akatuswalisha rakaa mbili-mbili mpaka tukarudi) [Imepokewa na Nasai.].

Makusudio ya Safari

Kila kinachoitwa safari kikawaida, basi hiyo ni safari ya kufaa kupunguza Swala

Kupunguza Swala

1. Msafiri ataanza kupunguza Swalah baada ya kupita makazi ya mji anaokaa. Na haruhusiwi kupunguza Swala na hali yeye yuko kwenye mahali pa makao yake, kwa kuwa haikuthibiti kuwa Mtume ﷺ alipunguza swala isipokuwa baada ya kutoka kwake.

2. Msafiri anapowasili kwenye mji na akanuilia kukaa hapo siku nne au zaidi, basi itamlazimu kutimiza. Na akinuilia kukaa chini ya siku nne, ataruhusiwa kupunguza. Na iwapo hakunuilia kukaa muda maalumu, lakini akawa na lengo ambalo akilimaliza atarudi, basi huyo anafaa kupunguza, hata kama muda utapita siku nne.

3. Inamlazimu msafiri kutimiza anaposwali nyuma ya imamu ambaye ni mkazi wa mji, hata kama hakuwahi kuswali na yeye isipokuwa rakaa moja.

4. Anaposwali mkazi wa mji nyuma ya msafiri anayepunguza Swala, itamlazimu kutimiza Swala yake baada ya imamu kupiga Salamu.

Kukusanya Swala mbili

1. Inafaa kwa msafiri na mgonjwa kukusanya baina ya Adhuhuri na Alasiri katika wakati wa Swala mojawapo. Akizikusanya katika wakati wa Swala ya kwanza itakuwa ni mkusanyo wa kutanguliza, na akizikusanya katika wakati wa Swala ya pili itakuwa ni mkusanyo wa kuahirisha.

2. Inafaa kwa anayeswali msikitini kujumuisha kukiwa na mvua yenye kusababisha usumbufu na matatizo. Ama anayeswali nyumbani kama vile wanawake, haruhusiwi kujumuisha.

3. Si lazima kujumuisha na kupunguza kuwe pamoja, kwani huenda akajumuisha na akafupisha, na huenda akajumuisha na asifupishe.

Swala ya msafiri akiwa garini

1. Iwapo ni swala ya sunna:

Swala itakuwa sahihi, awe na udhuru au asiwe na udhuru, kwa hadithi iliyothubutu kwamba Mtume ﷺ alikuwa akiswali sunna juu ya mnyama popote anapoelekea) [ Imepokewa na Bukhari.].

2- Iwapo ni swala ya faradhi:

Swala itakuwa sahihi iwapo hawezi kushuka kuswali chini, au akawa atashindwa kupanda akishuka, au akawa anaogopa adui au mfano wake. Na kuswali juu ya kipando kuna namna kadha, miongoni mwazo ni:

a. kuwa anaweza kuelekea Kibla na anaweza kurukuu na kusujudu, kama akiwa ndani ya jahazi. Hapo itamlazimu kuswali kwa namna yake inayojulikana, kwa kuwa anaweza.

b. aweze kuelekea Kibla na asiweze kurukuu na kusujudu. Hapo itamlazimu kuelekea Kibla wakati wa kupiga takbiri ya kufungia Swala, kisha ataswali vile gari litakavyomuelekeza na ataashiria kwa kurukuu na kusujudu.

3. Swala ya hofu

Swala ya Hofu imewekwa na Sheria katika kila mapigano ya halali, mjini au safarini, Na dalili ya kuwa imewekwa na Sheria ni Qur›ani na Sunna:

1. Katika Qur’ani ni neno lake Aliyetukuka: {Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao, na watakapo maliza sijida zao, basi na wende nyuma yenu, na lije kundi jengine ambalo halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao.} [4: 102].

2. Na katika Sunna ni kitendo cha Mtume ﷺ kwa kuwa yeye aliswali na maswahaba zake, pia waliiswali Swala hiyo baada yake.

Namana ya kuswali Swala ya Hofu

Hofu ya vita haina athari yoyote juu upunguzaji idadi ya rakaa, Swala ikiswaliwa mjini huswaliwa kama ilivyo, na ikiswaliwa safarini hupunguzwa, isipokuwa namna yake ina tofauti. Na kuhusu namna ya kuiswali kuna njia kadhaa ambazo zote zinafaa.

Na hofu yenye kupasisha Swala hii ina mojawapo ya hali mbili:

Hali ya Kwanza: Hali ya kuogopa kushambuliwa na adui:

Inaswaliwa kwa namna mojawapo ya namna zilizokuja kutoka kwa Mtume ﷺ. Na namna iliyotangaa zaidi ni ile iliyokuja kwenye hadithi iliyopokewa na Sahl bin Abi Hathmah t. Nayo ni kuwa imamu awagawanye makundi mawili. Kundi moja lisimame upande wa adui ili kulinda, na Kundi lingine litaswali pamoja na yeye rakaa moja. Anaposimama imamu kwenda kwenye rakaa ya pili, lile Kundi litanuilia kutomfuata imam na litajitimizia Swala yake na litatoa Salamu, kisha litakwenda upande wa adui kulinda. Hapo litakuja Kundi la kwanza, litaswali pamoja na imamu rakaa ya pili. Na imamu anapokaa kwa kikao cha Atahiyatu, watu wa Kundi lile watainuka na wajiswalie wenyewe, hali ya kuwa imamu anawangojea, na wanapomaliza kukaa kikao cha Atahiyatu imamu atapiga Salamu na wao.

Hali ya pili: ni pale hali ya hofu ikizidi na ikitowezekana kuswaliwa kwa namna ya kawaida iliyowekwa na Sheria:

Katika hali hii wataswali wakiwa wanatembea kwa miguu au wanapanda wanyama na kuelekea Kibla ikiwezekana, na ikitowezekana, basi wataelekea upande wowote ule, kama alivyosema Ibnu ‹Umar t: (Kukiwa na hofu kubwa zaidi wataswali wakiwa wanatembnea kwa miguu au wanapanda, wawe wameelekea Kibla au hawakuelekea) [ Imepokewa na Bukhari.], na wataashiria katika kurukuu na kusujudu. Ataswali naye anatembea au amepanda ndege yake au kifaru chake kwa hali inayomkinika, kama ilivyo katika hali ya vita na mapambano au katika hali nyiginezo ambazo mtu hua hamakiniki kuswali kwa namna yake ya kawaida. Na inaashiria hukumu hiyo neno lake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: (Mkiwa katika hali ya hofu, basi swalini mkiwa mnatembea kwa miguu au mko juu ya vipando) [2: 239].

Ataswali ndani ya kifaru
Ataswali ndani ya jahazi
Ataswali ndani ya ndege
Usahali na wepesi wa Sheria
Miongoni mwa sifa za Sheria Ya Uislamu za kipekee ni usahali na upesi na kuondoa dhiki. Na huu ni msingi ulioenea katika Sheria "Shida zinaleta usahali".