Hukumu za Swala

19216

 

1. Swalah ya mwenye kukaa

a. Katika Swalah ya Sunna:

Swala ya mwenye kukaa ni sahihi na thawabu zake ni nusu ya zile za mwenye kuswali kwa kusimama, kwa kuwa Mtume (S.A.W) alisema: (Akiswali kwa kusimama, basi hivyo ni bora. Na mwenye kuswali kwa kukaa basi thawabu zake ni nusu ya thawabu za mwenye kusimama. Na mwenye kuswali kwa kulala, basi thawabu zake ni nusu ya thawabu mwenye kukaa) [ Imepokewa na Bukhari.].

Na akiswali kwa kukaa kwa dharura, basi atapata thawabu kamili, kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Mja akiwa Mgonjwa au akiwa safarini, basi ataandikiwa thawabu mfano wa thawabu ya yale mema ambayo alikuwa akiyafanaya alipokuwa mjini na kuwa mzima) [ Imepokewa na Bukhari.].

b. Katika Swalah ya Faradhi:

Mwenye kuswi kwa kukaa hali yakuwa anaweza kusimama swala yake haikubaliwi

2. Kutia nia

Miongoni mwa hukumu za nia:

1. Haifai kuikata nia katikati ya Swala. Yoyote mwenye kutia nia ya kukata Swala, basi Swala yake huharibika na analazimika kuianza upya.

2. Mwenye kufunga Swala ya Sunna haitafaa kuigeuza katikati yake kuifanya Swala ya faradhi.

3. Mwenye kufunga Swala ya fardhi akiwa ana swali peke yake kisha ikakimiwa Swala ya jamaa, inafaa aigeuze nia yake kuifanya ni Swala ya sunna na akamilishe rakaa mbili kisha apige Salamu na aswali pamoja na jamaa.

3. Kusoma Suratul Fatiha

Ni lazima kwa mwenye kuswali kusoma Fatiha, katika Swala ya kujihirisha (kusoma kwa sauti), hata kama ni maamuma. Ubadah bin Swamit  alisema: (Tulikuwa nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ katika Swala ya Alfajiri, akasoma Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ, na kisomo kikawa kizito kwake. Alipomaliza Mtume ﷺ, alisema: (Huenda nyinyi mnasoma nyuma ya imamu wenu? Wakasema: ‘Ndio, tunafanya hivyo, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu’. Akasema ﷺ: “Msifanye hivyo isipokuwa kwa Ufunguzi wa Qur’ani (Fatiha), kwani asiyeisoma huwa hana Swala) [ Imepokewa na Abu Daud.].

4. Kusema ‹Aamiin›

Kusema ‹Aamiin’ ni sunna kwa kila mwenye kuswali, awe ni imamu au maamuma au mwenye kuswali peke yake au mwenye kuswali faradhi au mwenye kuswali Swala ya sunna, ziwe ni katika swala za kusoma kwa siri au za kusoma kwa sauti.

Dalili yake ni neno la Mtume ﷺ: (Imamu akisema ‘Aamiin’, basi na nyinyi semeni ‘Aamiin’. Kwani yoyote yule ambaye Amina yake imeafikiana na Amina ya Malaika, atasamehewa dhambi zake zilizotangulia) [Imepokewa na Bukhari.]

5. Vinyamazo vya imamu

1. Kinyamazo baina ya takbiri na kisomo kwa ajili ya dua ya kufungia Swala.

2. Kinyamazo baina ya Fatiha na Sura. Maamuma atasoma Fatiha katika vinyamazo vya imamu.

3. Kinyamazo baada kumaliza kisomo kabla ya kurukuu.

6. Kusoma kwa sauti wakati wa kukidhi Swala ya Faradhi, na Swala za sunna

Ikimpita Swala na akataka kuilipa: je, atasoma kwa siri au atasoma kwa sauti?

Linalozingatiwa ni ile Swala yenyewe, na sio wakati wa kuilipa, kwani lau anailipa Swala ya kusoma kwa sauti katika kipindi cha mchana, atatakiwa asome kwa sauti.

Sunna ni kusoma kwa siri katika Swala za sunna isipokuwa kunapokuwako dalili ya kusoma kwa sauti, kama vile Swala ya Tarawehe na Swala ya kupatwa kwa mwezi.

7. Kuinua mikono

Mikono huinuliwa katika sehemu zifuatazo:

1. Takbiri ya kufungia Swala.

2. Takbiri ya kurukuu.

3. Wakati wa kuinuka kutoka kwenye rukuu.

4. Wakati wa kuinuka baada ya kikao cha Atahiyatu ya kwanza.

8. Kuipata rakaa

Maamuma anapoiwahi rukuu pamoja na imamu, basi huwa ameipata rakaa, kwa kauli yake Mtume ﷺ: (Mwenye kuwahi Rukuu, basi huyo ameipata Rakaa) [ Imepokewa na Abu Daud.].

9. Kujituliza

Kujituliza katika nguzo zote za Swala ni mojawapo ya nguzo za hiyo Swala ambayo bila hiyo Swala haiwi sahihi. Hii ni kwa hadithi iliyopokewa na Abu Hurairah kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliingia msikitini. Kisha akaja mtu akaingia akaswali, kisha akaja akampigia Salamu Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ, na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺakamrudishia salamu. Akasema kumwambia: “Rudi uswali kwani wewe hukuswali”. Yule mtu akarudi akaswali kama alivyoswali. Kisha akaja kwa Mtume ﷺ akampigia salamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akasema kumjibu: “Na wewe salamu zikushukie” kisha akasema: “Rudi uswali kwani wewe hukuswali” [ Imepokewa na Bukhari.].

10. Kutingisha ulimi

Haitoshi katika kusoma Qur, ani, na kupiga takbiri na kutoa dhikri, kisomo cha moyoni, bali hapana budi kutamka. Na uchache wake ni kutikisa ulimi na mdomo kwa kisomo.

11. Namna ya kusujudu

Kusujudu kunakuwa kwa viungo saba kwa neno lake Mtume ﷺ: (Mja anaposujudu vinasujudu pamoja naye viungo saba: uso wake, vitanga vyake viwili vya mkono, magoti mawili yake na nyayo mbili zake) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

12. Kuashiria kwa kidole

Sunna ni kuashiria kidole katika kikao cha Atahiyatu., kwa hadithi ya Waail bin Hujr: (Kisha akainua kidole chake nikamuona akikitingisha, akiomba dua kwacho) [Imepokewa na Nasai.].

Yasiofaa

- Kutowa sauti wakati wa kutia nia na kulazimisha kufuata nia wakati wa kupiga takbiri ya kufungia swala.

- Kuzidisha neno (Washukru) wakati wakusema (Rabbanaa walakal Hamdu) na ziada hii haikupokewa kutoka kwa Mtume (SAW)

- Kuzidisha neno la (Sayyidnaa) katika Attahiyatu, au katika kumswalia Mtume (SAW) Katika Swala

- Kuashiria kwa mkono wa kulia upande wa kulia na kwa mkono wa kushoto upande wa kushoto wakati wa kutoa salamu

- Kupeana mikono baada ya kuswali,na kusema Haram,na mwengine kusema Jama’an na Mfano wake

- Wanavo fanya baadhi ya wenye kuswali kusoma mmoja wao Ayatul kursi kisha kusema: Subhana llah na wao wakaleta nyuma yake Tasbihi

- Kupangusa Uso baada ya Dua na Dhikri