Adhana na ikama

40804

 

Maana ya Adhana na Ikama

Kuadhini

Ni kujulisha kuingia wakati wa Swala kwa kuleta maneno maalumu ya dhikiri.

Kukimu

Ni kujulisha kuanza kuswaliwa kwa kuleta maneno maalumu ya dhikiri.

Hukumu ya kuadhini na kukimu

1. Katika Swalah za jamaa:

Ni faradhi ya kutosheleza, kwa Swalah tano za faradhi peke yake, safarini na mjini, kwa kuwa hizo mbili ni miongoni mwa alama za Uislamu za waziwazi, hivyo basi haifai kuziacha. Amesema Mtume ﷺ: (Ufikapo Wakati wa Swala, basi awaadhinie mmoja wenu, kisha awaswalishe mkubwa wenu) [ Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

2. Katika Swalah ya anayeswali peke yake:

Ni sunna. Amepokewa ‹Uqbah bin ‹Amir akisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema: (Anamuonea ajabu Mola wako mchunga mbuzi aliye juu ya kilele [ Shadhiyyah: Ni kipande kilichoinuka kilichoko kwenye kilele cha jabali.] cha jabali, anayeadhini kwa Swala kisha akaswali, hapo aseme Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Mwangalieni mja wangu huyu, anaadhini kisha anakimu Swala, ananiogopa! Nishamsamehe mja wangu na nitamuingiza Peponi”) [ Imepokewa na Annasai.].

Hikma ya kuadhini

1. Kujulisha kuwa wakati wa swala umeingia.

2. Kuhimiza juu ya Swalah ya jamaa.

3. Kuwazindusha walioghafilika na kuwakumbusha waliosahau watekeleze Swalah ambayo ni miongoni mwa neema tukufu zaidi.

Adhana imewekwa lini na sharia na ni kwa sababu gani?

Adhana iliwekwa na Sheria mwaka wa kwanza wa Hijria. Na sababu yake ni kuwa ilipotokea haja ya kuweka alama ambayo kwayo watu wote watajua kuwa wakati wa Swala umeingia Waislamu walishauriana juu ya hilo. Ulipokuja usiku Abdullah bin Said aliota usingizini kuwa amemuona mwanamume amebeba kengele[ Naaquus: kengele.], Akamwambia: “ je, unauza kengele hii?” Yule mwanamume akasema: “Wataka kufanyia nini?”. Abdullah akasema: “Tuwaitie watu kwenye Swala”. Yule mwanamume akasema: “Je, sikupi ushauri wa kitu bora kuliko hiki?” [ Imepokewa na Daarimi.].

Abdullah akasema: “kwani? Nipe”. Hapo akamfundisha adhana hii ijulikanayo, kisha akamfundisha ikama. Abdullah alisema: Nilipopambaukiwa nilimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ nikampa habari ya kile nilichokiona usingizini. Akasema ﷺ: (Hiyo ni ndoto ya kweli, Mwenyezi Mungu Akitaka, basi inuka pamoja na Bilali umfudishe hayo maneno, kwani yeye ana sauti kubwa zaidi kuliko wewe) [ Imepokewa na Abu Daud.].

Fadhla za kuadhini

1. Kinamtolea ushahidi mwadhini kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, kila kilichofikiwa na sauti yake. Amesema Mtume ﷺ: (Hakuna jini wala binadamu wala kitu chochote kinachofikiwa na sauti ya mwadhini isipokuwa humshuhudilia Siku ya Kiyama) [ Imepokewa na Bukhari.].

2. Lau watu wangejua ubora wa kuadhini wangalishindaniana kwa hilo. Amesema Mtume ﷺ: (Lau watu wanajua ubora ulioko kwenye adhana na safu ya mbele, kisha wasipate suluhisho isipokuwa wapige kura [ Isthaam: Kupiga kura ili apatikane anaestahiki kutangulizwa.], basi wangepiga kura kushindania hayo) [ Imepokewa na Bukhari.]

Masharti ya kuswihi kwa adhana

1. Muadhini awe ni Muislamu, mwanamume, mwenye akili.

2. Adhana ilingane na mpango uliowekwa.

3. Iwe ni yenye kufuatanishwa, kusiwe na mwanya mrefu baina ya maneno yake.

4. Iwe ni pale unapoingia wakati wa Swala.

Sunnah za kuadhini

1. Kuelekea Kibla.

2. Kutwahirika kwa mwadhini kutokana na hadathi mbili.

3. Kuzunguka katika ha-yaa Ala(Swala/Falaa) mbili, nazo ni anaposema: Ha-yaa Ala Swalat. Ha-yaa Alal Falah, kuliani na kushotoni.

4. Mwadhini aweke vidole vyake viwili vya shahada masikioni mwake.

5. Mwadhini awe na sauti nzuri ya nguvu.

6. Adhana itolewe kwa ufafanuzi na utulivu.

Namna ya kuadhini na kukimu

1. Namna ya kuadhini: (Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Allaahu akbar. Ash’hadu an laa ilaaha illa Allah, Ash’hadu an laa ilaaha illa Allah.Ash’hadu anna Muhammadan Rasuulu-Allah, Ash’hadu anna Muhammadan Rasuulu-Allah, Hayya ‘ala ssalaah, Hayya ‘ala ssalaah. Hayya ‘ala l falaah, Hayya ‘ala l falaah. Allaahu Akbar, Allaahu Akbar. Laa ilaaha illa Llaah) [ Imepokewa na Muslim].

2. Namna ya kukimu: (Allaahu Akbar, Allaahu Akbar. Ash’hadu an laa ilaaha illa Llaah. Ash’hadu anna Muhammadan Rasuulu Laah. Hayya ‘ala l falaah. Allaahu Akbar, Allaahu Akbar. Laa ilaaha illa Llaah).

Yanayopendekezwa kwa anayesikia adhana

1. Asema kama vile anavyosema mwadhini, isipokuwa anaposema: (Haya njooni mswali! Haya njooni kwenye kufaulu !) hapo atasema (Hapana hila zozote za kufanyia mambo ya utiifu wala nguvu zozote za kuyaepuka maasia isipokuwa ni kwa msaada wa Mwenyezi Mungu) [ Imepokewa na Bukhari.].

2. Asema baada ya adhana: (Nashuhudilia kwamba hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Hana mshirika, na kwamba Muhammad ni mja wake na Mtume Wake. Nimeridhika kwamba Mwenyezi Mungu ndie Mola, na kwamba Muhammad ﷺ, ni mtume na kwamba Uislamu ni Dini) [ Imepokewa na Muslim.].

3. Amswalie Mtume ﷺ baada ya adhana, kisha aseme: (Ewe Mola! Bwana wa ulinganizi huu uliotimia, na Swala hii iliyosimama! Mpe Muhammad njia za kheri na utukufu, na umfikishe kwenye Cheo chenye kusifiwa ulichomuahidi) [ Imepokewa na Abu Daud.].

Miongoni mwa hukumu za Adhana na Ikama

1. Adhana peke yake inatosha wakati wa kukusanya Swala mbili, kama vile Adhuhuri na Alasiri, Na hapo kutakimiwa kwa kila Swala.

2. Swala ikikimiwa, kisha kukachelewa kuswaliwa, basi hakuna haja ya kukimiwa mara ya pili.

3. Ni juu ya mwadhini ajihadhari na kukosea katika matamshi ya adhana, na miongoni mwayo ni:

a. kusema “Aallaahu Akbar?” kwa kuuliza swali.

b. Kusema: “Allaahu akbaar” kwa kuivuta Baa.

c. kusema: “Allaahu wa akbar” kwa kuzidisha Waw.

4. Swalah ikikimiwa, haifai kuswali swalah ya sunnah. Ama ikiwa itakimiwa na mtu ashaanza kuswali Sunna, ataikamilisha iwapo imesalia kidogo kumalizika, na ikitokuwa hivyo, ataikata, bila ya kutoa Salamu, na ataingia kwenye Swala ya faradhi pamoja na imamu.

5. Adhana ya mtoto anayefahamu inakubalika

6. Sheria imeweka adhana na ikama kwa Swala iliyompita mtu kwa sababu ya kulala au kusahau, kwa hadithi iliyothubutu kwa Mtume ﷺ walipolala Maswahaba wakapitwa na Swala ya Asubuhi mpaka jua likachomoza, kwamba alimuamuru Bilali akaadhini, kisha wakatawadha na wakaswali rakaa mbili za Alfajiri, kisha akamuamuru Bilali akimu Swala, akakimu Swala na Mtume akawaswalisha Swala ya Asubuhi ) [ Imepokewa na Ahmad.].

7. Aliye msikitini baada ya kuadhiniwa hafai kutoka isipokuwa kwa dharura, kwa hadithi iliyopokewa na Abu Hurairah t alisema: ( Alituamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kwamba mkiwa msikitini na mwadhini ukaadhiniwa, asitoke mmoja wenu mpaka aswali) [ Imepokewa na Ahmad.]

8. Mwadhini anatakiwa na Sheria ateremshe sauti yake katika shahada mbili, kisha arudie kuongeza sauti, kwa kuwa hilo limethubutu katika Sunna. [ Imepokewa na Abu Daud.]

Yasiofaa

1. kuleta adhana kwa mahadhi na kuimba kwa namna inayopelekea kugeuza herufi, haraka, sakna, kupunguza na kuzidisha.

2. kuinua sauti kwa kumswalia Mtume ﷺ baada ya adhana.

3. Kusema, baada ya kusikia: QAD QAAMATU SWALAAT “Swala imesimama”: “Mwenyezi Mungu Aisimamishe na Aidumshe”, bali atalirudia neno hilo kama lilivyo.

- Adhana ya Swala ya Alfajiri

Alfajiri imewekewa adhana mbili: ya kwanza ni kabla ya kuingia wakati, na ya pili ni ya kujulisha kuwa wakati umeingia ili watu wahudhurie kuswali. Katika adhana ya kwanza, mwadhini anatakiwa aseme: “Swala ni bora kuliko kulala” mara mbili, kwa kuwa Mtume ﷺ alisema: Ukiadhini adhana ya kwanza ya Alfjiri, sema: “Swala ni bora kuliko kulala “ [ Imepokewa na Abu Daud.]

Adhana Humfukuza Shetani
Kutoka kwa Abuu hurera (RA) amesema: Amesema Mtume ﷺ (Inapo Nadiwa kwa ajili ya swala shetani hukumbia na huku akishuta, ili asisikie Adhana inapo malizika Adhana hurudi, inapo kimiwa hukimbia inapo malizika hurudi na kuingia kati ya mtu na nafsi yake, na kumwabia: kumbuka kitu Fulani na Fulani, jambo ambalo alikuwa halikumbuki, mpaka mtu akawa hajui ameswali ngapi, asipojuwa mmoja wenu ameswali rakaa ngapi, tatu au nne, basi asujudu sijida mbili na hali yakuwa amekaa) [ Imepokewa na Bukhari.]
Faida

1. Haifai kutoka Msikitini baada ya kuadhiniwa na kabla ya kukimiwa kwa hadithi ya Abuu Hureyra (RA) Alipo muona mtu ametoka Msikitini baada ya kuadhiniwa, akasema: ama huyu amemuasi babake Qaasim (SWA)

2. Hakuadhiniwi wala hakukimiwi kwa Swala ya sunna, wala Swala ya Iddi Mbili, wala Swala ya Jeneza, ila katika Swala ya Kupata kwa jua kutanadiwa Swalatu Jaamia

3. wakati wa Mvua nyingi au ubaridi kali atesema Muadhini bada ya hayyalal falah Alaa Swalluu fi Rihalikum (Swalini majumbani mwenu)