Jinsi Ya Kuondosha Najisi Ya Mbwa Kwenye Nguo

SWALI: Swali langu ni kwamba, Je hii najis inaondoshwa vipi ya mbwa? na je akininusa juu ya nguo sio kwenye ngozi inabidi nikoshe zile nguo tu au na mimi mwenyewe nijikoshe? na je inanuiwa vipi wakati wa kujikosha na kuiondosha hii najsi ya mbwa? Natumai swali langu litawanufaisha waislamu wenzangu wengi hasa wanaoishi nchi za nje. Naomba tafadhalini munijibu haraka iwezekananyo kwani nategemea kuanza kazi pahala ambapo pana mbwa karibuni inshAllaah!!!

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu kwa swali lako. Ama kuhusu najisi inayopatikana kwa kunuswa na mbwa basi maelezo ni kama yafuatayo. Pahali paliponajisiwa kwa kurambwa na mbwa au kunuswa kama chombo na kadhalika mfano huo. Ili kitu hicho kutwaharika na kusafishika na kurudi katika hali yake ya kawaida na usafi kinatakiwa kioshwe mara saba mojawapo kwa mchanga. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Anaporamba mbwa kwenye chombo cha mmoja wenu, basi akioshe mara saba, mojawapo kwa mchanga" (Muslim, Ahmad na Abu Daawuud). Ikiwa amenusa kwenye nguo utaiosha nguo tu kwa mchanga na maji ikiwa hakuna taklifa, la sivyo unaweza kutumia sabuni na maji hususan ikiwa utafua nguo hiyo kwa mashine ya kufulia nguo, na akiwa amenusa ngozi yako basi utaiosha hiyo sehemu ya ngozi kwa maji na mchanga mara saba. Pia unaweza kutumia sabuni pamoja na maji. Niyah ya kila kitu iko moyoni, hivyo ukishanuia moyoni mwako kuondosha najisi inatosheleza kabisa, huna haja kutamka wala kusema maelezo au kuyahifadhi. Bonyeza viungo vifuatavyo kupata elimu zaidi: Mbwa Wa Kufuga Je, Ni Najsi? Hukmu Ya Manyoa Ya Mbwa Anayefugwa Nyumbani Jinsi Ya Kuondosha Najisi Ya Mbwa Kwenye Nguo Na Allaah Anajua zaidi
Vitambulisho: