Imaam Ibn Baaz - Hukmu Ya Swalaah Ya Mwenye Mashaka Kuwa Katokwa Na Upepo

SWALI: Ninapoingia kwenye Swalaah, yananijia mawazo kuwa nimetokwa na upepo, lakini sisikii sauti wala harufu. Lakini, wakati ninahisi hivyo, mimi najidhibiti na kuizuia nafsi yangu hadi Swalaah inamalizika; je, nini hukmu juu yangu?

JIBU: Aliulizwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu ambaye ana kitu (upepo unataka kumtoka kwenye tupu yake) katika Swalaah, akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 'Asiondoke (asikate Swalaah) hadi asikie sauti au apate harufu.' Na katika lafdhi nyingine ya Hadiyth: 'Atakapopata mmoja wenu kitu katika tumbo lake, ikamtatiza yeye, je, kuna kitu kimetoka au hapana? Asitoke katu mtu huyo Msikitini mpaka asikie sauti au apate harufu.' Na kile ambacho kinampitikia yeye (mawazoni) kuwa anatokwa na kitu, hakibatilishi wudhuu wake na Swalaah yake, bali yeye atabaki katika hali yake ya usahihi wa wudhuu, na Swalaah yake ni sahihi. Na pindi atakapojua kwa yakini kuwa ametokwa na upepo au mkojo, twahaarah yake itabatilika na Swalaah yake itabatilika. Ama ikiwa tu ni mashaka aliyonayo, basi Swalaah yake na wudhuu wake ni sahihi; kwani huo ni wasiwasi tu wa Shaytwaan. [Fataawaa Samaahat Ash-Shaykh Ibn Baaz, mj. 29, uk. 339]
Vitambulisho: