Ufafanuzi Wa Swali La Kumlipia Mama Aliyefariki Deni Swawm

SWALI: asalam alaykum mimi ni yule msichana ambae niliuliza swala kuhusu kumlipia mama yangu ambae ameshafariki swaumu yake huyu mama yangu hii swaumu ilipitiwa na miezi kumi na tatu na yeye alikuwa hai je tunaweza kumlipia ule ule mwezi mmoja au naomba munieleze tutalipa vipi au inaongezeka nisaidieni huyu mama yangu alihafilika na hakulilipa deni lake kwa muda mrefu M/mungu awape afya na nguvu muzidi kutusaidia

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunashukuru dada yetu kuhusu swali lako jingine la kutaka ufafanuzi kuhusu jibu tulilotoa kwako katika mas-ala ya kumlipia funga mama yako aliyeaga dunia. Awali ya yote ni muhimu tufahamu kuwa katika kulipa deni ikiwa ni lako au unamlipia mama mzazi tuwe ni wenye kufanya hima kulipa kabla Ramadhaan nyingine haijafika. Ikiwa utakuwa umepitia vyema jibu letu la mwanzo suala hili halingekuwa limejitokeza kwani limo ndani. Kwa ufupi ni kuwa nyinyi kama watoto wa aliyefariki mnatakiwa mumlipie mama yenu zile siku za Ramadhaan ambazo hakuweza kuzifunga. Ikiwa ni mwezi mzima mnafaa mfunge mwezi. Ikiwa mtamtolea na sadaka juu ya funga (yaani mkamfungia na kumtolea sadaka) itakuwa kheri zaidi kwa mama yenu. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na atakayefanya wema kwa radhi ya nafsi yake, basi ni bora kwake. na huku kufunga ni bora kwenu ikiwa mnajua” [2: 184]. Tunatumai tutakuwa tumeeleweka vizuri kuhusu hilo. Na Allaah Anajua zaidi
Vitambulisho: