Nguzo za swaumu na ya kuharibu swaumu

32912

 

Nguzo za swaumu

NGUZO YA KWANZA: Ni kujizuia kufanya mambo yatakayo Haribu swaumu kuanzia kutokeza kwa alfajiri hadi kuzama kwa jua kwa kuingia jioni

Dalili ni kauli yake Mwenyezi Mungu U: {…Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni saumu mpaka usiku…} (Al-Baqarah- Aya 187).

NGUZO YA PILI: Ni kutia nia ya Kufunga

Nako ni kukusudia kwa anayefunga saumu ya kwamba huku kujizuia na vitu vinavyofungua saumu ni ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwa dalili ya kauli ya Mtume (saw): ( Hakika kila jambo analolifanya (mwanadamu) ni kulingamana na nia yake, na hakika kila mtu atalipwa kulingana na alivyonuilia) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

Mambo yanayofaa kufanya ndani ya swaumu

1. Kuoga, na kukaa mahali penye maji ili kupata baridi.

2. Kumeza mate na makohozi.

3. Kuonja chakula ili kujua kiwango cha sukari au chumvi yake kwa kutumia ulimi peke yake, kwa sharti asiingize chochote katika chakula hicho hadi kwenye koo.

4. Kunusa harufu ya manukato na visafisha hewa.

Matumizi ya mswaki kwa mtu aliyefunga
Yaruhusiwa kutumia mswaki kwa mtu aliyefunga wakati wowote ule, sawasawa iwe ni kabla ya kuzama kwa jua kwa kuingia jioni au baada ya hapo, na vilevile uwe mswaki wenyewe uko majimaji au mkavu, lakini anatahadharishwa aliyefunga ikiwa mswaki anaotumia uko majimaji kusije kukaingia chochote kooni wakati anapiga mswaki; kwa sababu kuingia kwa kitu kooni kunaharibu saumu yake.

Mambo yanayopendekezwa kufanywa ndani ya saumu

1. Kula daku na kuchelewesha kula daku hadi karibu sana na kuadhiniwa alfajiri

Kwa kauli ya Mtume (saw): (Kuleni daku, hakika katika kula daku kuna Baraka) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

Na inahesabika kula daku kwa kupatikana chakula kingi au kidogo, hata kama ni tama la maji kwa kauli ya Mtume (saw): “Daku uchache wake ni baraka, basi msiache kula daku, hata kama atakunywa mmoja wenu tama la maji, kwani Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanawaswalia wenye kula daku” [Imepokewa na Ahmad.]

Na inapendekezwa kuchelewesha kula daku, kutoka kwa Zaid ibn Thaabit t Anasema: (Tulikula daku pamoja na Mtume ﷺ, kisha tukasimama kuswali (yaani swala ya alfajiri), anasema Anas ibn Malik: nikasema: ilikuwa ni kipindi cha mda gani kati ya kula kwenu hiyo daku na kuswali? Akasema: kiwango cha (kusoma) Aya hamsini) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

- Kunywa wakati adhana inapo adhiniwa

Mtu anaposikia adhana na kinywaji chake kipo mkononi mwake basi anaruhusiwa kunywa hadi amalize; kutoka kwa Abu Hureirah anasema: Amesema (saw): “Atakaposikia mmoja wenu adhana na hali ya kuwa chombo cha kunywea maji kipo mkononi mwake basi asikiweke kando mpaka amalize haja yake ya kutumia hicho chombo” [Imepokewa na Abuu Daud.]

Na wanazuoni wamesema kuhusu hadithi hii ni kwa Yule ambae ana shaka kutokeza kwa alfajiri, ama akihakikisha kuwa alfajiri imetokeza kwa huyu hafai kuendelea kula wala kunywa, na akiendelea kufanya hivyo Saumu yake imebatilika na itamlazimu Ailipe

2. Kufanya haraka katika kufungua saumu

Yapendekezwa kwa aliyefunga kufanya haraka kufungua saumu yake pindi tu anapohakikisha kwamba jua limezama na kuingia jioni.; kwa kauli ya Mtume (saw): (Watu wangali katika kheri pindi wanapoharakisha kufungua saumu zao) [Imepokewa na Abuu Daud.].

Na inapendekezwa mtu kufungua saumu kwa rutab (tende tosa), asipopata rutab basi afungue kwa tende, na hizo tende ziwe ni hesabu isiyogawanyika kwa mbili (kama vile tende moja, tatu, tano na mfano huu), asipopata tende basi na anywe matama ya maji; kulingana na hadithi ya Anas ibn Malik, anasema: “Alikuwa Mtume (saw) anafungua saumu kwa Rutab (Tende Tosa) kabla hajaswali, na ikiwa hakuna Rutab basi alikuwa akifungua kwa tende kidogo hivi, na ikiwa hakuna tende alikuwa akinywa [ Hasaa: alikunywa.] matama ya maji” [Imepokewa na Tirmidhi.].

Na akiwa hakupata kitu chochote cha kufungulia saumu basi atanuia kufungua saumu kwa moyo wake, na hili litamtosheleza kwamba amefungua.

Atakae Funguwa kwa bahati mbaya

Atakapo kula mtu aliyefunga hali ya kudhania kwamba jua limezama na kuingia jioni, au kwa kutoelewa kutokeza kwa alfajiri, kisha ije kum’bainikia kinyume na alivyodhania, basi haimlazimu kwake kuilipa saumu hiyo; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu U: { Wala si lawama juu yenu mkikosa, lakini (kuna lawama) katika yale ziliyoyafanya nyoyo zenu kwa kusudi } ( Al-Ahzab- Aya 5).

Na kauli yake Mtume (saw): “Hakika ya Mwenyezi Mungu amewaondoshea umma wangu (hawaandikiwi madhambi) kwa jambo watakalolikosea bila ya kukusudia na kwa watakayofanya kwa kusahau, na kwa watakayolazimishwa kufanya (hali ya kuwa wao wenyewe wanayachukia)” [ Imepokewa na Ibnu Maajah.]

3. kuomba Dua wakati wakufungua swaumu

Kwa ilivyo Thubutu kutoka kwa Mtume (saw) Alipokuwa akifunguwa Saumu Akisema: “Kiu imeondoka, na jasho limekuwa majimaji (limeanza kutokeza), na yamepatikana malipo (ya thawabu) apendapo Mwenyezi Mungu” [Imepokewa na Abuu Daud.].

Na amesema Mtume (saw): “Hakika kwa aliyefunga saumu wakati anapofungua kuna dua isiyorudi) [ Imepokewa na Ibnu Maajah.] yaani dua inayokubalika moja kwa moja mbele ya Mwenyezi Mungu U.

4. Kuacha mambo ya upuzi na mambo machafu

Kwa kauli ya Mtume (saw): “Ikiwa ni siku ambayo mmoja wenu amefunga, basi asifanye mambo machafu, [ Yarfuth Kufanya mambo machafu: yatokamana na neno uchafu, nako ni kutamka matamshi mabaya, na vile vile hutumika neno hili kumaanisha tendo la ndoa na vitangulizi vya tendo hili.] wala asikemee wenziwe[ Yaskhab: Yuwakemea: yatokamana na neno kemea, nako ni kubishana na kupiga ukulele.], anapotukanwa na mtu, au anapopigwa vita basi na aseme: Mimi ni mtu niliyefunga” [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

(Yaani ajitahidi kujiepusha kupigana na kutukanana na watu).

Na kwa neno lake Mtume (saw) (Asie acha maneno machafu na kuyatumia basi Mwenyezi Mungu hana haja kwa mtu huyo kuacha chakula chake na kinywaji chake) [Imepokewa na Abuu Daud.]

5. Kuzidisha kwa wingi kufanya Ibada

Kama kusoma Qur’an, na kufanya adhkari kumtaja Mwenyezi Mungu, na kuswali swala ya Tarawehe, na visimamo vya usiku (swala za usiku wakati watu wamelala), na kufanya visimamo vya usiku wa Lailatul Qadri, na kuswali swala za sunnah, na kutoa sadaka, na kuwa mkarimu na kujitahidi katika kufanya mambo ya kheri, na kuwalisha waliofunga wakati wa kufungua saumu zao, na kwenda U’mrah, kwasababu matendo mema siku ya Ramadhani malipo yake yanaongezeka mara nyingi sana, kutoka kwa Ibn Abbas anasema: “Alikuwa Mtume (saw) ni mkarimu kushinda watu wote, na alikuwa mkarimu zaidi wakati wa Ramadhani pindi anapokutana na Jibril, na alikuwa Jibril akikutana na Mtume kila usiku wa mwezi wa Ramadhani, ikawa anamfundisha Qur’an (yaani Jibril anamfundisha Mtume Qur’an), basi Mtume (saw) pindi anapokutana na Jibril alikuwa mkarimu katika mambo ya kheri kushinda upepo mkali uliotumwa” [Imwpokewa na Bukhari.].

6. Kujitahidi kwa Ibada hasa kumi lamwisho katika Mwezi wa Ramadhani

Imepokewa na bibi A’isha t Amesema: (Alikuwa Mtume (saw) likingia kumi la mwisho akijifunga kibobwe [(Shadda mi’zarah) Nikinaya cha mtu kujitihidi katika ibada zaidi kuliko ilivo zowewa. Na kumesemwa ni kinaya cha mtu kujiepusha na mkewe, Almi’zar: ni kikoi nacho nikile kinchovaliwa sehemu chini ya muili.] na akiuhuisha usiku na akiwamsha wakezake[(Ayqadha Ahlahu) akiwatanabahisha kwa ajili ya ibaada na akiwahimiza juu yake.]) [Imwpokewa na Bukhari.]

Mambo yanayochukizwa kuyafanya ndani ya saumu

1. Kupitisha mpaka katika kusukutuwa na kupandisha maji puani

Na hii ni kwa ajili ya kuhofia maji yasije yakaingia tumboni mwake, kwa kauli ya Mtume (saw): “Na fanyeni sana katika kupandisha maji puani isipokuwa wakati mtu amefunga saumu” [Imwpokewa na Abuu Daud.].

2. Kumpiga busu kwa matamanio ya kimapenzi

Inachukizwa kwa aliyefunga saumu ikiwa anachelea nafsi yake kutokwa na manii au kusisimukwa kwa matamanio ya kimapenzi.

Na ni juu ya aliyefunga kujiepusha na kila ambalo kwamba litampelekea kusisimukwa na kuleta harakati za kuibuka matamanio ya kimapenzi, na ikiwa anaamini nafsi yake kwamba haitompelekea katika hisia za matamanio ya kimapenzi basi hakuna kosa kwake kum’busu mkewe au mke kumbusu mumewe; kutoka kwa A’isha anasema: “Alikuwa Mtume(saw) akipiga busu na kubashiriana ( yaani akimshikashika mkewe), na alikuwa ni m’bora zaidi kuliko nyinyi katika kumiliki matamanio ya kimapenzi [ Irbihi: Haja yake.]” [Imwpokewa na Bukharin a Muslim.].

Na kwa ajili hii inachukizwa kubashiriana kimapenzi kwa kijana kinyume na mzee kwa kuwa kijana damu yake ni moto zaidi, kutoka kwa Abu Hureirah anasema: “Kwamba kuna mtu mmoja alimuuliza Mtume (saw) kuhusu kubashiriana mke na mume kwa aliyefunga, Mtume akampa ruhusa ya kufanya hivyo, na akaja mwengine akauliza (swali hilo hilo), Mtume akamkataza, kwani yule aliyempa ruhusa alikuwa ni mzee, na yule aliyemkataza alikuwa ni kijana” [ Imwpokewa na Abuu Daud.].

Mambo yanayoharibu Saumu

1. Kula na kunywa kwa kukusudia ndani ya mchana wa Ramadhani

Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu U: {Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni saumu mpaka usiku} (Al-Baqarah – Aya 187).

Kula kwasababu ya kazi
Yoyote anayefanya kazi mahali pa mapishi ya mikate hivi na mahali pa kazi ngumungumu sio ruhusa kwao kutofunga (yaani hawafai kula mchana wa Ramadhani); kwasababu wamelazimika kama watu wengine kufunga Ramadhani.

- Maelezo

- Atakaye kula au kunywa kwa kusahau basi saumu yake imeswihi (iko sawa haina tatizo lolote), na inamlazimu kujizuia na vitu vinavyoharibu saumu pindi anapokumbuka; kwa kauli ya Mtume (saw): “Aliyesahau hali ya kuwa amefunga akala na kunywa, basi akamilishe saumu yake, kwani Mwenyezi Mungu amemlisha na kumnywesha (mtu huyo)” [Imwpokewa na Muslim.].

- Kinaharibu saumu chochote kile kinachoingia tumboni kwa njia ya mdomoni au puani, na chochote kinachofahamika kuwa chakula au kinywaji, kama vile sindano za lishe/chakula. Ama sindano ambazo si za chakula, kama penicillin na mfano wake, hazifunguzi saumu, kwasababu sio chakula wala kinywaji, wala sio kwa maana ya chakula.

- Chochote kinachoingizwa mdomoni kwa ajili ya kutizama kitu na vipuliza hewa vya kutibu pumu na mfano kama huu, hakiharibu saumu.

- Wanja, na matone ya kitu majimaji kutonezwa kwenye jicho na sikio na mfano wa hivi viwili havivunji saumu, kwasababu hakuna dalili ya vitu hivi kuharibu saumu, na kwasababu jicho sio sehemu inayotegemewa kwa kuingilia chakula na kinywaji, na vile vile matone ya kitu majimaji kwenye sikio na puani, lakini ubora kwa haya matone ni kujitenga nayo, kwa jinsi alivyokataza Mtume (saw) kuhusu kupita mpaka katika kupandisha maji puani kwa aliyefunga, [Imwpokewa na Tirmidhi.] na kwasababu ni sehemu inayopitisha chakula hadi tumboni.

- Anapotumia mtu kitu ambacho hakiliwi au kinadhuru, kama vile sigara basi atakuwa amefungua, kwasababu amekitumia kupitia sehemu inayotumika kwa chakula, nayo ni mdomo, kama nayo itakavyofahamika kuwa chakula ama kinywaji.

- Hakiharibu saumu kitu ambacho kwamba huwezi kukiepuka, kama vile vumbi la njiani, na mabaki ya chakula yaliosalia kati ya meno.

Dawa inayotumika kama chakula inaharibu saumu.
Sindano ya penicillin haiharibu saumu.(Hii ni sindano ya kukinga au kutibu madhara yanayosababishwa na bacteria).
Vipuliza hewa vya kutibu pumu haviharibu saumu.
Wanja haiharibu saumu.
Sigara zinaharibu saumu.
Mabaki ya chakula yaani katika meno hayaharibu saumu.

2. Kufanya Tendo la Ndoa

Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu U { Mmehalalishiwa usiku wa saumu kuingiliana na wake zenu} (Al-Baqarah – Aya 187).

Na “Ar-Rafath” ni neno la kiarabu lililotumika katika Aya hii kumaanisha kuingiliana – yaani kufanya tendo la ndoa, basi yoyote atakaye ingiliana na mkewe au mumewe hali ya kuwa amefunga, saumu yake itakuwa imeharibika, na atalazimika ailipe siku hiyo, na pamoja na kuilipa ni juu yake kutoa kafara nzito, nayo ni kuacha huru mtumwa, akiwa hatopata mtumwa wa kumuacha huru, atalazimika kufunga miezi miwili mfululizo, na akiwa hawezi kufunga atalazimika kulisha masikini sitini, kama ilivyothibiti kutoka kwa Abu Hureiah t Anasema: “ Alikuja mtu mmoja kwa Mtume (saw) akasema nimeangamia. Mtume akamuuliza: Una nini? Akajibu: Nimemuingilia mkewangu ndani ya Ramadhani. Mtume akamuuliza: Waweza kuacha mtumwa huru?. Akajibu: Siwezi.. Mtume akamuuliza: je waweza kufunga miezi miwli mfululizo? Akasema: Siwezi. Mtume akamuuliza: Basi waweza kulisha masikini sitini?. Akasema: Siwezi. Mtume akamwambia: Kaa. Akakaa. Mtume (saw) akaleta chombo ambacho ndani yake mna tende. Akasema: Chukua (hiki chombo) wende ukatolee sadaka. Akasema yule mtu: Je kuna fakiri zaidi yetu? (yaani maskini kuliko familia yake). Mtume akacheka mpaka yakaonekana magego ya meno yake, akasema: Lisha familia yako ( hizo tende)” [Imwpokewa na Bukharin a Muslim.].

Na inakuwa kafara inafuata mfumo huu, hivyo basi mtu asilishe maskini isipokuwa akiwa hawezi kufunga hiyo miezi miwili mfululizo, wala asifunge isipokuwa ikiwa hawezi kuacha huru mtumwa.

Na inamlazimu mwanamke kutoa kafara ikiwa ameridhiana na mumewe kufanya tendo la ndoa, na iwapo amelazimishwa na mumewe kuingiliana basi saumu yake imeharibika na itamlazimu mwanamke huyo kuilipa saumu hiyo peke yake bila ya kutoa kafara.

Na ni katika maana ya jimai (tendo la ndoa) kujitoa manii kwa kukusudia, Mtu akitokwa na manii kwa kubusiana, au kwa kugusa au kwa kutumia mkono, basi saumu yake itaharibika, kwa sababu hiyo ni katika shahawa inao haribu saumu, na itakuwa ni juu yake kuilipa saumu yake wala hatolazimika kutoa kafara, kwa sababu kafara imekuja kwa tendo la ndoa peke yake.

Mtu akibusu au akigusa au akifikiria akatokwa na madhii saumu yake ni swahihi. kwa kutokuwa na dadili yakuharibu saumu kwa kutokwa na madhi

Mtu anapo lala akaota, au akatokwa na manii bila ya shahawa kama kuwa mgonjwa, saumu yake ni swahihi kwa sababu hayakutoka kwa hiyari yake.

Mtu anapo amka na janaba la tendo la ndoa kabla ya alfajiri au akaota, saumu yake ni swahihi na ni juu yake kuoga ili apate kuswali alfajiri na jamaa, imethubutu kutoka kwa bibi A’isha t Kwamba Mtume ﷺ Alikuwa akiingiliwa na Alfajiri na yeye akiwa na janaba la mkewe, kisha akioga na akifunga

3. kujitapisha kwa kusudi

Nao ni mtu kutoa kilichoko tumboni kutokana na chakula au kinywaji kwa njia ya mdomo kwa kusudi, ama akishindwa na akatoka bila ya khiyari yake haiathiri saumu yake kwa neno lake Mtume (saw) ( Mwenye kushindwa na matapishi basi hana haja ya kukidhi na mwenye kujitapisha kwa kusudi basi alipe)

4. Damu ya Heidhi na Nifasi

Wakati wowote mwanamke atakapo ona damu ya hedhi au nifasi japo kuwa ni wakati wa jioni kabla ya kutwa jua kwa mda mchache saumu yake itaharibika na atawajibika kuilipa

Faida

- Kauli yenye nguvu ni kuwa kuumika hakuvundi saumu kwa sababu Mtume (saw) Aliumika na hali yakuwa amefunga, Amepokewa kutoka kwa said Al’khudriy t akisema (Aliruhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ Kubusu kwa aliyefunga na kuumika, lakini inachukizwa kuumika kwa ajili ya kudhofika, Aliulizwa Anas bin Maalik t Mulikuwa mukichukiza kuumika kwa alie funga? Akasema la ila kwa ajili ya kudhofika.

- Haidhuru mtu kutokwa na damu katika jaraha, au kung’oa jino au kutokwa na damu za puwa, au kutoa damu kwa ajili ya kujipma, au kujitolea, yote haya hayaharibu swaumu.Vitambulisho: