Itikafu(kukaa ndani ya msikiti)

9509

 

 

Maana ya Itikafu

Itikafu ki-lugha.

Ni kujilazimisha na jambo fulani, na kujifunga nafsi yako juu ya kulifanya jambo hilo.

Itikafu ki-sheria.

Ni kujilazimisha kukaa ndani ya msikiti kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Usharia wa Itikafu

Kufanya itikafu ni katika matendo yaliyo bora sana, na twa’a tukufu. Kutoka kwa A’isha Mungu awe naye radhi anasema: “Alikuwa Mtume (saw) akifanya itikafu (maisha yake) katika kumi la mwisho wa mwezi wa Ramadhani mpaka Mungu alipomkabidhi roho yake (Mtume alipokufa)” [Imepokewa na Bukhari.].

Na inaruhusiwa ki-sheria kwetu sisi na kwa waliokuja kabla yetu kufanya itikafu, Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: ( Na tulimusia Ibrahimu na Ismaili Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wanaoizunguka kwa ajili ya kutufu na wanaokaa hapo na (kwa ajili ya) wanaorukuu na kusujudu hapo pia”) ( Al-Baqarah –Aya 125).

Hukumu ya Kukaa Itikafu

Kufanya itikafu ni sunna wakati wowote ule, na ubora wake zaidi kuifanya ni katika kumi la mwisho wa mwezi wa Ramadhani; kwasababu Mtume ﷺ alidumu katika kufanya itikafu kwenye kumi la mwisho wa mwezi wa Ramadhani [Zaadul-Ma’ad.].

Masharti ya Kukaa Itikafu

1. Kutia niya.

Mwenye kufanya itikafu anatia niya ya kujilazimisha kukaa ndani ya msikiti kwa lengo la kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kumuabudu; kwa kauli ya Mtume (saw): ( Hakika kila Amali ni kwa niya ya mtu) [Imepokewa na Bukhari na Muslim].

2. Msikiti atakaofanyia Itikafu uwe ni msikiti wa kuswali swala ya jumaa.

Haifai kufanya Itikafu isipokuwa Msikitini kwa neno lake Mwenyezi Mungu ( Hali yakuwa mumekaa itikafu msikitini) [Al-baqara: 187]

Na kwa kitendo chake Mtume (saw) kwani hakufanya Itikafu isipokuwa Msikitini.

Na kufanya itikafu msikiti usio swaliwa Jamaa itampelekea Mwenye kufanya Itikafu kutoka mara kwa mara kuenda kuswali jamaa kwa sababu Swala ya jamaa kwake ni wajibu, na kule kutoka mara kwa mara hukosekana maana ya Itikafu, ama mwanamke husihi Itikafu yake msikiti wowote sawa uwe msikiti waswaliwa jamaa au hauswaliwi, na hii ni ikipelekea kutopatikana fitna katika kukaa kwake itikafu, ama ikipatikana fitna haifai na atakatazwa.

Na ubora uwe msikiti unaswaliwa swala ya ijumaa lakini hilo si katika masharti ya itikafu

3. Kuwa twahara kutokamana na hadathi kubwa.

Haifai kwa mwenye janaba kufanya Itikafu, wala mwenye damu ya heidhi, wala mwenye damu ya nifasi, kwa kule kukosekana kwao ruhusa ya kukaa ndani ya msikiti.

Kufunga sio Sharti ya Kukaa Itikafu.

Haizingatiwi kufunga kama ni sharti ya kukaa Itikafu. Kwasababu imepokewa kutoka kwa Ibn Umar kwamba Umar alimuuliza Mtume (saw) akisema: Niliweka nadhiri wakati wa Jahiliya (kabla ya kuwa Muislamu) kwamba nifanye Itikafu usiku mmoja ndani ya Masjid haram. Mtume (saw) akasema: ( Basi itekeleze nadhiri yako [Imepokewa na Bukhari.].

Lau ingekuwa kufunga ni sharti ya kufanya Itikafu basi isingekubalika Itikafu ya Umar kufanya usiku. kwasababu usiku watu hawafungi. Na imethibiti vile vile kwamba Mtume (saw) alifanya Itikafu katika kumi la kwanza la mwezi wa Shawwal [Imepokewa na Muslim.], na katika kumi hili kuna masiku ya Idi ambayo mtu hafai kufunga, kama vile vile (saumu na Itikafu) ni ibada mbili ambazo hazikuambatana pamoja, kwa hivyo sio lazima kufanya nyingine kwa kupatikana mojawapo.

Wakati wa kukaa Itikafu

Yaruhusiwa kufanya Itikafu siku yoyote ile, na wakati wowote ule, isipokuwa ubora wake ni isipunguwe Itikafu mchana mzima au usiku mzima; kwasababu haijapokewa kutoka kwa Mtume (saw) wala kutoka kwa yoyote katika maswahaba zake ambaye alifanya chini ya hapo.

Kukaa Itikafu katika kumi la Mwisho la Mwezi wa Ramadhani

- Nao ndio wakati bora zaidi wa mtu kufanya Itikafu, kama ilivyithibiti kutoka kwa A’isha t kwamba Mtume (saw) alikuwa akifanya Itikafu kwenye kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani mpaka alipokufa [Imepokewa na Bukhari].

- Na yoyote atakayenuia kufanya Itikafu katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani ataswali alafajiri ya kuamkia tarehe ishirini na moja katika msikiti atakaofanya Itikafu, kisha ndio aanze Itikafu yake. Imepokewa kutoka kwa A’isha Mungu awe naye radhi akisema: (Alikuwa Mtume (saw) akifanya Itikafu kila mwezi wa Ramadhani, na pindi anaposwali swala ya asubuhi alikuwa akienda mahali pake ambapo atafanyia Itikafu yake) [Imepokewa na Bukhari.].

- Na inamalizika Itikafu kwa kuzama kwa jua siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani, na ubora ni kuondoka kutoka kwenye Itikafu mapema sana asubuhi ya siku ya Idd, na ndivyo ilivyothibiti kwa wengi watu wema waliotangulia.

Hikima ya kufanya Itikafu.

Hikima iliyoko katika Itikafu ni kujikatisha na mambo ya kidunia na kutojishughulisha nayo na watu wake, na kujitengea mda maalumu kwa ajili ya ibada, basi inamlazimu mwenye kufanya Itikafu kuutengea moyo mambo haya.

Mambo yanao ruhusiwa kufanywa ndani ya Itikafu

1. Kutoka msikitini pasipo na budi kufanya hivyo, kama kutoka kwa ajili ya kula na kunywa, ikiwa hana mtu wa kumletea chakula, na kutoka ili kukidhi haja zake (kwenda choo), kama ilivyothibiti kutoka kwa A’isha akisema: (Alikuwa Mtume (saw) pindi anapofanya Itikafu akiinamisha kichwa chake kuja kwangu nikimchana nywele, na alikuwa hatoki nje isipokuwa kwa haja ya kibinadamu) [Imepokewa na Muslim.].

2. Kutengeza nywele zake vizuri na kuzichana; kama ilivyopokewa kwa Hadithi iliyopita.

3. Kuzungumza na watu maneno yenye faida, na kuwajulia hali zao, lakini hairuhusiwi kuzidisha katika kujuliana hali, kwasababu ni kinyume cha makusudio ya Itikafu.

4. Watu wake na jamaa zake kumzuru, na kutoka mahali pake pa Itikafu ili kuwaaga jamaa zake. Imepokewa kutoka kwa Swafiya Binti Huyay – Mungu awe naye radhi anasema: “Alikuwa Mtume (saw) yuko kwenye Itikafu nikaenda kumtembelea siku moja nikamuinamia (kuongea naye) kisha nikasimama ili niende zangu, akasimama pamoja nami ili kunisindikiza” [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

Mambo yenye kuharibu Itikafu

1. Kutoka msikitini bila ya dharura yoyote kwa kukusudia – hata kama kipindi ulichotoka ni kichache kiasi gani -;

Kama ilivyothibi kutoka kwa A’isha t akisema: (Na alikuwa (Mtume) haingii nyumbani isipokuwa kwa haja ya kibinadamu) [Imepokewa na Muslim.].

Na kwasababu kule kutoka kuna acha kipindi fulani kukosekana kwa mwenye kufanya Itikafu ndani ya msikiti, na huku kuwa ndani ya msikiti ni nguzo ya Itikafu.

2. Kufanya tendo la ndoa – hata kama kufanya huko kutakuwa ni usiku.

Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu U: {Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu misikitini} (Al-Baqarah – Aya 187).

Na hukumu hii ya tendo la ndoa pia inasimamia: Kuondosha matamanio bila ya kuingiliana kama kujitoa manii kwa kutumia mkono, na kumshikashika mkeo sehemu zisizo za siri.

3. Kuwa na niya ya kuivunja Itikafu.

Anaponuia Muislamu kufanya Itikafu siku maalumu, kisha akavunja kuifanya hiyo Itikafu yuwafaa ailipe, kama ilivyothibiti kutoka kwa A’isha – Mungu awe naye radhi asema: (Alikuwa Mtume (saw) anapotaka kufanya Itikafu akiswali alfajiri kisha ndio aingie mahali pake pa itikafu [ Mahali pake pa Itikafu: Yaani sehemu anayokaa kufanyia Itikafu.]. Na hakika aliamrisha kufungwa khibai (hema) lake na likafungwa – Hali ya kutaka kufanya Itikafu kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani -; Zainab naye aliamrisha kufungwa khibai lake na likafungwa. Na aliamrisha mwengine katika wake za Mtume (saw) kufungwa khibai lake na likafungwa. Mtume alipomaliza kuswali alfajiri akatizama, akaona makhibai (mahema). Akasema: Ni wema munataka? Akachukua khibai lake akalinyanyua [ Kulinyanyua: Yaani kulikunjakunja lile khibai.]. Na akaacha Itikafu katika Ramadhani mpaka kumi la kwanza la mwezi wa Shawwal” [Imepokewa na Bukhari na Muslim]. Na katika upokezi mwengine: (kumi la mwisho la mwezi wa Shawwal).

4. Mwenye kufanya Itikafu hatembelei mgonjwa wala hashindikizi jeneza.

Na yuwabaki kufanya ibada mahali pake pa Itikafu.Vitambulisho: