Kupiga Mswaki Kwa Mkaa

SWALI: NDUGU ZANGU KWA IMAN NAWASHUKURU SANA TENA SANA KWA KAZI YENU INSHAALLAH M.MUNGU HATA WATUPA, BISMILLAH, NILIKUWA NA ULIZA KWA BAADHI YA WATU WAKISEMA KUWA MAKAA UKITAFUNA AMA KUSUGULIA MENO INATAKATISHA NA MAJIVU PIA LAKINI WENGI WANADAI NI DHAMBI WANGINE WASEMA KATIKA KITABU YA MATIBABU IMESEMA IKICHUKUA SUKARI MAKAA NA ASALI INASAFISHA MENO NDUGU ZANGU WA IMAN NIAMBIENI JEE IMETHIBITI KWA MTUME S.A.W. NATARAJI NAMI MUNITUMIE KTK EMAIL YANGU SHUKRAN WA FIAMANILLAH

JIBU: AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa muulizaji swali kuhusu mas-ala haya ya kutumia mkaa kusafisha meno. Hakika ni kuwa katika kufanya tiba ipo atahri kubwa ya kuondoa balaa na kupata ponyo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alihimiza pale aliposema: "Kila ugonjwa una dawa, ikisibu dawa ugonjwa unapona kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka " (Muslim na Ahmad kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah [Radhiya Allaahu 'anhuma]). Na pia Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana upigaji wa mswaki mpaka akatueleza kuwa lau haingekuwa shida kwa Ummah wake basi angelazimisha upigaji wa mswaki kabla ya kila Swalah ya faradhi (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy kutoka kwa Zayd bin Khaalid al-Juhaniy [Radhiya Allaahu 'anhu]). Sunnah hii ya kupiga mswaki ni katika fitwrah ya mwanaadamu na hasa Muislamu anafaa afuate hizo. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema: " Mambo kumi ni katika fitwrah (maumbile ya asli ya Kiislamu): 'Kupunguza masharubu, kufuga ndevu, kupiga mswaki, kupitisha maji puani (kusafisha), kukata kucha, kusafisha penyo za vidole, kung'ofoa (kunyoa) nywele za kwapa, kunyoa nywele za sehemu za siri, na kujisafisha kwa maji baada ya kujisaidia na msimuliaji akasema kasahau la kumi, lakini inaweza kuwa ni kusafisha mdomo (kusukutua) " (Muslim na Abu Daawuud kutoka kwa Bibi 'Aa'ishah [Radhiya Allaahu 'anha ]). Hivyo tunaona kuwa utumiaji wa mswaki umehimizwa sana katika Uislamu kwani ni njia ya kuweka usafi wa kwinywa na mdomo wa mtu. Na mas-ala ya usafi Uislamu umeyapatia kipaumbele sana. Ama kuhusu swali lako ukweli ni kuwa haifai Muislamu kutumia mkaa kwa shughuli ya kujitwahirisha nayo kutokana na haja ndogo au kubwa kwa mujibu wa Hadiyth ifuatayo ikiwa maana ya neno humamah litachukuliwa kuwa ni mkaa: " Uwakilishi wa Majini ulikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: 'Ewe Muhammad! Wakataze Ummah wako wajisafishie na mfupa au mavi ya (hayawani) au humamah, kwani kwayo Allaah Ametupatia riziki yetu. Hivyo, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akakataza utumiaji (wa vitu hivyo)" (Abu Daawuud kutoka kwa 'Abdullaah bin Mas'uud [Radhiya Allaahu 'anhu]). Waumbuji wa lugha wanatuambia kuwa humamah ni mkaa, jivu au takataka. Kwa hiyo, mbali na kuwa tumekatazwa kutumia mkaa kwa kujitwahirishia ikiwa imechukuliwa maana hiyo kuwa ndio ya neno humamah hakuna tatizo kusafishia meno ikiwa hayo uliyosema kuwa yanaleta natija nzuri ni kweli. Na Allaah Anajua zaidi.
Vitambulisho: