Swalaah Ya Safari Inaadhiniwa na Kukimiwa?

SWALI: swali langu ni1. ni kiwali swala safar inabidi nikiikmu na kuadhini?.

JIBU: AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. Ni jambo linaloeleweka kuwa Swalaah ya safari ni kama Swalaah ya mkaazi ila kwa tofauti chache. Tofauti ni kuwa Swalaah ya safari zinajumuishwa na kupunguzwa (rakaa nne kuwa mbili). Kwa ajili ya kujumuisha hizo Swalaah Adhana inakuwa moja badala ya mbili lakini Iqaamah zinabaki mbili vile vile kama kawaida. Kufanya hivyo ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Jaabir bin Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswalisha Swalaah mbili ‘Arafah kwa Adhana moja na Iqaamah mbili… Kisha akaja Muzdalifah akaswali ndani yake Maghrib na ‘Ishaa’ kwa Adhana moja na Iqaamah mbili, wala hakuleta adhkaar baina yake, kisha akalala mpaka ikatoka Alfajiri …” [Muslim, Abu Daawuwd, Ibn Maajah na ad-Daarimiy]. Kwa hiyo, Sunnah katika kujumuisha Swalaah mbili ni kuadhini Adhana moja na kuleta Iqaamah kwa kila Swalaah. Na Allaah Anajua zaidi
Vitambulisho: