Swalah iliyowekwa na Sheria isiyokuwa ya lazima
Swalah iliyowekwa na Sheria isiyokuwa ya lazima
1. Swala ya sunna ni sababu ya mja kupendwa na Mwenyezi Mungu. Imekuja kwenye hadithi Alqudusiy kwamba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ansema: (Haachi mja wangu kuendelea kujikurubisha kwangu kwa sunna mpaka nimpende, na ninapompenda nitakuwa ni masikizi yake ya kusikia na maangalizi yake ya kuonea na mkono wake wa kushikia na mguu wake wa kuendea, na akiniomba nitampa, na akijilinda kwangu nitamlinda) [Imepokewa na Bukhari.]
2. Swala ya sunna inaunga kasoro za faradhi. Mtume (s.a.w) amesema: (Kitu cha kwanza wanachohesabiwa kwacho Siku ya Kiyama miongoni mwa matendo ni Swala. Mwenyezi Mungu aliyetukuka, Atawaambia Malaika wake- na yeye ni mjuzi zaidi-: “Itizameni Swala ya mja wangu, je ameikamilisha au ameipunguza?” Iwapo imekamilika inaandikwa kuwa imekamilika, na ikiwa ina upungufu wa kitu, Atasema: “Tizameni, je mja wangu huyu ana sunna alizoziswali? Akiwa ana sunna, Atasema: Mkamilishieni mja wangu faradhi yake kutoka kwa sunna zake” ) [Imepokewa na Abu Daud.].
3. Swala ya sunna nyumbani ni bora zaidi
Swala ya sunna majumbani ni bora kushinda misikitini isipokuwa katika Swala ziliwekewa jamaa na Sheria kama Swala ya Tarawehe katika mwezi wa Ramadhani. Mtume (s.a.w) amesema: (Bora zaidi wa Swala ya mtu ni ile anayoiswali nyumbani kwake isipokuwa Swala ya faradhi) [Imepokewa na Bukhari.].
Swala ya sunna ni aina nyingi: Muhimu zaidi ya hizo ni zifuatazo:
Nazo ni sunna zenye kufuata Swala za faradhi
Na jumla ya sunna za ratiba ni rakaa kumi au rakaa kumi na mbili, nazo ni:
- Rakaa mbili kabla ya Alfajiri.
- Rakaa mbili kabla ya Adhuhuri au nne na rakaa mbili baada yake.
. Rakaa mbili baada ya Magharibi.
- Rakaa mbili baada ya Isha. Ibnu ‹Umar amepokewa akisema: (Nimehifadhi kutoka kwa Mtume (s.a.w) rakaa kumi: Rakaa mbili kabla ya Adhuhuri na rakaa mbili baada yake, rakaa mbili baada ya Magharibi nyumbani kwake, rakaa mbili baada ya Isha nyumbani kwake na rakaa mbili kabla ya Swala ya Asubuhi) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na imethubutu hadithi kama hii kutoka kwa ‘Aishah t isipokuwa yeye alitaja rakaa nne kabla ya Adhuhuri [Imepokewa na Muslim.].
Sunna ya Qabliya | Swala za faradhi | Sunna ya Baadiya |
Rakaa 2 | Alfajiri | ــــــــ |
Rakaa 4 | Adhuhuri | Rakaa 2 |
ــــــــ | Alasiri | ــــــــ |
ــــــــ | Magharibi | Rakaa 2 |
ــــــــ | Ishaa | Rakaa 2 |
Na bora wa sunna za ratiba ni ambazo Mtume (s.a.w) alidumu nazo mjini na safarini ni rakaa mbili za Alfajiri, kwa hadithi ya ‹Aishah t kwamba alisema: (Mtume ﷺ hakuwa akidumu na kitu chochote miongoni mwa sunna isipokuwa rakaa mbili za Alfajiri) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na imesunniwa kuzifanya fupi rakaa zake bila kuziharibu wajibu wake, kwa ilivyothubutu kutoka kwa Aishah t kuwa alisema: (Alikuwa Mtume (s.a.w) akizifupisha zile rakaa mbili za kabla ya Swala ya Asubuhi kwa kiasi kwamba nilikuwa nikisema: “Je amesoma Fatiha?”) [Imepokewa na Bukhari.].
Imethubutu Ubora wa kuswali rakaa nne baada ya swala ya adhuhuri, kwa neno lake Mtume (s.a.w) : ( Mwenye kuswali kabla ya Adhuhuri rakaa nne na baada yake rakaa nne Mwenyezi mungu atamuharamishia moto) [Imepokewa na Abu Daud.]
- Na katika Swala za Sunna zisizo tiliwa mkazo, ni kuswali rakaa nne kabla ya Alasiri, kwa neno lake Mtume (s.a.w) (Mwenyezi Mungu amrehemu mja alie Swali kabla ya Alasiri Rakaa nne) [ Imepokewa na Abu Daud.]
-Inafaa kuswali sunna zisizo kutiliwa mkazo, kabla ya Alasiri na Magharibi na ishaa, kwa neno lake Mtume (s.a.w) (Kati ya kila Adhana mbili kuna swala, alisema mara tatu na alisema mara ya tatu kwa anaetaka) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Na makusudio ya Adhana mbili: ni Adhana na Ikama.
-Inafaa kukidhi swala ya sunna akitomakinika kuiswali kwa sababu ya usingizi ama kwa kusahau, hata kama ni wakati ulio katazwa kuswali, kwa ilivyo thubutu kutoka kwa Mtume (s.a.w) Aliposhughulishwa aliswali Sunna baadiya ya Adhuhuri baada ya swala ya Alasiri.
Witri ni sunna iliyotiliwa mkazo. Mtume (s.a.w) anasema: (Hakika Mwenyezi Mungu ni Mmoja, Anapenda Swala ya Witri basi Swalini Witri enyi watu wa Qur’ani ) [Imepokewa na Abu Daud.].
Na alikuwa Mtume (s.a.w) akidumu nayo akiwa mjini na akiwa safarini
1. Uchache wa Swala ya Witri ni rakaa moja na wingi wake ni rakaa kumi na moja au kumi na tatu, anaziswali mbilimbili kisha anaswali moja ya kufanyia witri.
2. Na uchache wa ukamilifu ni rakaa tatu, ataswali rakaa mbili kisha atowe Salamu, kisha ataswali rakaa moja na atowe Salamu. Pia inafaa kwa mtu kuziswali hizo rakaa tatu kwa kikao cha Atahiyatu kimoja. Na inapendekezwa asome katika rakaa ya kwanza baada ya Fatiha sura ya Al-A’laa na katika rakaa ya pili sura ya Al-Kaafiruun, na katika rakaa ya tatu sura ya Al-Ikhlas, kwa hadithi iliyothubutu kutoka kwa ubayy bin Ka’b t kuwa alisema: (Alikuwa Mtume ﷺ akisoma katika rakaa ya kwanza ya witri ‘Sabbihisma Rabbikal A’laa’, na katika ya pili ‘Qul yaa ayyuhal kaafiruun’, na katika ya tatu ‘Qul Huwallaahu Ahad’) [Imepokewa na Nasaai.].
Ni baada ya Swala ya Isha mpaka kutokea wakati wa Alfajiri. Na kuiswali kipindi cha theluthi ya mwisho ya usiku ni bora zaidi, kwa Hadithi ya Jaabir (RA) kuwa Mtume (s.a.w) alisema: (Atakaechele kutoamka mwisho wa usiku basi aswali witr mwanzo wake) [ Imepokewa na Muslim.], wala hatoswali tena witr, kwa neno lake Mtume (s.a.w) (Hakuna witri mbili katika usiku mmoja) [ Imepokewa na Abu Daud.].
Na Amesema tena (Atakae kuwa nahamu yakuamka mwisho wa usiku, basi aiswali witr mwisho wake, hakika Swala ya mwisho wa usiku inashuhudiliwa, na hilo ni bora) [Imepokewa na Muslim.].
Sheria imeweka dua katika rakaa ya mwisho ya Witri kabla ya kurukuu [ Imepokewa na Abuu Daaud.] au baada ya kuinuka kutoka kwenye rukuu [Imepokewa na Bukhari.].
Atainua mikono yake na aombe dua zilizopokewa, na miongoni mwa dua hizo ni: (Ewe Mola! Niongoze niwe miongoni mwa wale uliowaongoza, Unipe afya niwe miongoni mwa wale uliowapa afya, Uninusuru niwe miongoni mwa wale uliowanusuru, Unibarikie katika kile ulichonipa, Uniepushie shari ya kile ulichokadiria. Hakika Wewe unaamua na huamuliwi. Hakika hadhaliliki uliyemfanya rafiki wala hatukuki unaeteta naye. Zimekithiri kheri Zako, ewe Mola wetu, na Umetukuka) [Imepokewa na Tirmidhi.].
Na imamu aletapo kunuti wataitikia maamuma Aamin katika dua ya maombi, ama katika dua yakumsifu Mwenyezi Mungu watanyamaza kama asemapo Hakika Wewe unaamua na huamuliwi
1. Sunna ni kusema baada ya Swala ya Witri: (Kutakasika ni kwa Mfalme Mtakatifu) [ Imepokewa na Ahmad.], mara tatu. Aivute sauti yake na aiinue juu mara ya tatu. Pia inafaa kuzidisha: (Mola wa Malaika na Jibrili) [Imepokewa na Tirmidhi.].
2. Kupangusa uso baada ya kuomba dua hakukuwekwa na Sheria, si katika Witri wala penginepo kwa kuwa hilo halikupokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w)
3. Nakunuti inafaa kwa mwaka mzima, wala haikhusishwi katika nusu ya mwisho wa mwezi wa ramadhani, na nisunna kukunutiwa katika swala za faradhi kunapo tokea majanga na kadhalika
4. Dua ya kukhitisha Dua ya kukhitimisha Qur’ani katika Swala haikuwekwa na sharia
Tarawehe ni Swala ya usiku katika mwezi wa Ramadhani.
Na imeitwa Tarawehe kwa kuwa wao walikuwa wakipumzika baada ya kila rakaa nne kwa sababu ya urefu wa Swala
Tarawehe ni sunna iliyotiliwa mkazo, iliwekwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) katika mwezi wa Ramadhani tukufu, kwa kuwa Nabii (s.a.w) aliiswali na swahaba zake msikitini masiku kadha, kisha akaacha kuiswali kwa kuogopa isifaradhiwe juu yao. Na maswahaba waliifanya baada yake ﷺ [Imepokewa na Muslim.].
Lililo bora zaidi ni rakaa kumi na moja, kwa kuwa hiko ndicho kitendo alichokuwa Mtume (s.a.w) akikifanya zaidi, Kwa kauli ya ‘Aishah t alipoulizwa: “Ilikuwa namna gani Swala ya Mtume?” Akasema: (Hakuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akizidisha katika Ramadhani au miezi mingine kupita rakaa kumi na moja) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
1. Swala ya usiku ni Sunna iliyotiliwa mkazo katika mwaka Mzima, Imekirihishwa kwa anayeswali usiku kuacha ada yake. Abdullah bin ‹Amr bin Al-›Aasw t alipokwea akisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) alisema: (Ewe Abdullah! Usiwe kama fulani aliyekuwa akiinuka usiku kuswali kisha akaacha kuinuka usiku) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
2. Imependekezwa kwa mtu akizundukana kwa kuswali usiku amuamshe mke wake, kadhalika mwanamke amuamshe mumewe, kwa kauli yake Mtume (s.a.w) : ( Mtu akimwamsha mke wake usiku wakaswali rakaa mbili pamoja, wataandikwa kuwa ni miongoni mwa wanaume na wanawake wenye kumtaja Mwenyezi Mungu) [Imepokewa na Abuu Daaud].
3. Mwenye kushindwa na usingizi katika Swala ya usiku, basi aiache Swala na alale mpaka usingizi umuondokee. ‘Aishah t alipokewa akisema kwamba Nabii (s.a.w) alisema: (Akisinzia mmoja wenu katika Swala, basi na alale mpaka usingizi wake umuondokee) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
4. Imependekezwa kuleta istighfari na kuomba dua katika theluthi ya mwisho ya usiku, kwa hadithi iliyopokewa na Abu Huraira t kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema: (Anateremka mwenyezi Mungu kwenye uwingu wa karibu katika kipindi cha theluthi ya usiku ya mwisho na Anasema: “Ni nani aniombae nimkubalie? Ni nani anayeniomba msamaha nimsamehe?) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Nayo ni Swala iliyowekwa na sheria kuswaliwa kipindi cha mwanzo wa mchana.
Na Wakati wa Swala ya Dhuha: Ni kuanzia pale jua linapochomoza na kuangatika kadiri ya uti wa mkuki. Kuangatika huku kunakuwa ni kiasi cha theluthi ya saa mpaka kipindi cha kabla ya jua kupinduka kwa uchache, wa robo saa au theluthi yake, na ubora wawakati ni pale jua linapokuwa kali zaidi.
Amesema Mwenyezi Mungu katika Hdithi qudsi (takatifu): (Ewe mwanadamu! Swali kwa ajili yangu rakaa nne mwanzo wa mchana, nipate kukutosheleza mwisho wake) [Imepokewa na Muslim.].
Yafaa kuswaliwa rakaa mbili au Nne au Sita au Nane, kwa kuwa Mtume (s.a.w) alifanya hivyo.
Na mwenye kuswali rakaa Nne Mwenyezi mungu atamtosheleza siku yake, Amepokea Nuaym bin Hammazi Al-ghatwafaniy kutoka kwa Mtume (s.a.w) Kutoka kwa Mola wake alietukuka kwamba yeye amesema (Ewe mwanadamu Swali kwa ajili yangu rakaa nne mwanzo wa mchana nitakutosheleza mwisho wake) [ [ Imepokewa na Ahmad.]
Na mwenye kuiswali baada ya kuswali Alfajiri kwa jamaa na akakaa kumtaja Mwenyezi Mungu mpaka jua likachomoza basi ataandikiwa ujira wa hijja na umra iliyo timia Amesema Mtume (s.a.w) (Mwenye kuswali swala ya asubuhi kwa jamaa kisha akakaa kumtaja mwenyezi mungu mpaka jua likachomoza kisha akswali rakaa mbili basi huandikiwa ujira wa hijja na umra ) akasema Mtume (iliyotimia iliyotimia iliyotimia) [Imepokewa na Tirmidhi na imeswahihiswa na Albaani katika Swahihul Jaami’i]
Nayo ni rakaa mbili imewekewa yule aliyeingia msikitini kabla hajakaa.
Na hukmu yake ni sunna iliyo tiliwa mkazo sana.
Na Dalili yake ni kauli ya Mtume (s.a.w) : (Akiingia mmoja wenu msikitini, basi aswali rakaa mbili kabla hajakaa) [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na inatosheleza badala yake sunna inayofuatana na faradhi. Mwenye kuingia msikitini kwa kuswali adhuhuri- kwa mfano- akaswali sunna ya adhuhuri itamtosheleza, na hatatakiwa kuswali Swala ya kuuamkia msikiti.
Nayo ni rakaa mbili ambazo mtu ataziswali anapokuwa katika hali ya kutoamua katika jambo, kabla ya kuchukua uamuzi juu yake, na huombwa Dua baada yake Na Mtume (s.a.w) alikuwa akiwafundisha Maswahaba Swala hiyo kama alivyokuwa akiwafundisha sura ya Qur›ani.
Amesema Mtume(s.a.w) (Akiwa na nia mmoja wenu ya kufanya jambo, basi na aswali rakaa mbili zisizokuwa za faradhi, kasha aseme: “Ewe Mola! Hakika mimi nakutaka shauri kwa ujuzi wako, nakuomba kwa uwezo wako na ninakuomba fadhila zako zilizo kubwa. Kwa hakika wewe unaweza na mimi siwezi, na unajua na mimi sijui, na wewe Ndiye Mjuzi wa ghaibu zote. Ewe Mola! Iwapo kwenye ujuzi wako wewe, jambo hili lina kheri na mimi katika dini yangu, maisha yangu na mwisho wa jambo langu, au alisema ‘mambo yangu ya sasa na ya baadae’ basi nikadiria na unifanyie sahali kisha unitilie baraka katika jambo hili. Na ikiwa kwenye ujuzi wako jambo hili lina shari na mimi katika Dini yangu, maisha yangu na mwisho wa jambo langu, au alisema ‘katika mambo yangu ya sasa na ya baadae’ niepushe nalo na liepushe na mimi. Na unikadirie kheri yote mahali iliyopo, kisha niridhishe nalo”. asema ‘Kisha aitaje haja yake’) [ Imepokewa na Bukhari.].
Kwa kuwa ilithubutu kutoka kwa Abu Huraira t kwamba Mtume (s.a.w) alimwambia Bilal wakati wa Swala ya Alfajiri: (Ewe Bilal! Nihadithie juu ya tendo jema ulilolifanya katika Uislamu unalolitarajia zaidi, kwani mimi nilisikia mchakato wa viatu vyako [ Daff na’laika: sauti ya viatu vyako.] Peponi) Akasema: (Sikufanya tendo jema lolote ninalolitarajia zaidi isipokuwa mimi wakati wowote ninapojitwahirisha ninaswali kwa utwahara huo vile ninavyokadiriwa, iwe ni kipindi cha mchana au usiku) [Imepokewa na Bukhari.].
Nayo ni Swala isiyofungamana na wakati wala sababu.
Na Swala ya sunna iliyoachiliwa inaruhusiwa kuswaliwa wakati wowote isipokuwa kwenye nyakati ambazo kuswali kumekatazwa.
Mtume (s.a.w) alisema: (Bora wa Swala baada ya faradhi ni Swala ya Usiku) [ Imepokewa na Muslim.].
Na pia alisema (s.a.w) : (Hakika Peponi kuna Vyumba huonekana nje kutoka ndani yake, na ndani yake kutoka nje yake). Akainuka Mbedui akasema “Ni vya nani hivyo?” Akasema: (Ni vya anayesema maneno mazuri, na akalisha chakula, na akadumu kufunga na akaswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu usiku na ilhali watu wamelala) [ Imepokewa na Tirmidhi.].
1. Kuanzia baada ya Swala ya Alfajiri mpaka kuchomoza jua na kuangatika kiasi cha urefu wa mkuki, ambao kwa kawaida inakuwa ni kiasi cha theluthi ya saa
2. kuanzia kipindi cha jua kuwa limesimama katikati mpaka lipinduke.
3. Kuanzia baada Swala ya Alasiri mpaka jua lizame.
Na dalili yake ni hadithi iliyopokewa na ‹Uqbah bin ‹Amir kuwa alisema: (Nyakati tatu, alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akitukataza kuswali, au kuzika[ Naqbura: twazika.] maiti zetu: wakati jua likichomoza [ Baazighah: wazi.] hadi liangatuke, wakati wa katikati ya mchana mpaka jua lipinduke na wakati jua linapopindukia[ Tudhayyafu: linapindukia.] kuchwa mpaka lizame) [ Imepokewa na Muslim.].