Surat Al-Faatihah Ikikosewa Kusomwa Na Imaam Swalaah Yake Au Za Maamuma Hubatilika?

SWALI: Asalam alaykum warrahmatullah wabarakat swali langu ni kwamba kukosea kuisoma vizuri surat FATIHA kunaharibu swala? na kama imam ndio kakosea kuisoma surat FATIHA, je swala za watu wanaomfuata pia zinaweza kuharibika?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu Suratul Faatihah kusomwa kimakosa na Imaam. Ni vyema Imaam anayeswalisha Waumini awe ni mjuzi wa kisomo na ndilo agizo la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Uimaam. Kutoka kwa Abu Mas’uud Al-Answaariyy amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Awaswalishe watu yule mwenye kujua kusoma zaidi Kitabu cha Allaah (Qur-aan) na wakiwa katika kusoma wako sawa, basi mwenye ujuzi zaidi wa Sunnah (Hadiyth), na wakiwa kwenye Sunnah wako sawa, basi aliyetangulia kuhama (Hijrah), na wakiwa wako sawa katika kuhama, basi mkubwa wao kwa umri, wala asiswalishe mtu katika nyumba yake wala katika mamlaka yake wala asikae kwa heshima yake isipokuwa kwa ruhusa yake.” Muslim Kusomwa suratul Faatihah ni nguzo katika Swaalah na kuswihi kwake, kwa minajili hiyo itakuwa vigumu kuwa na Imaam asiyeisoma vyema surah hiyo. Mara nyingine hutokea kuwa kusomwa vibaya kwa sababu aliyeswalishwa ndiye mbora katika hao waliopo. Ikiwa ni hivyo, Swaalah za wote zitakuwa ni sahihi bila ya tatizo. Au hutokea mara nyengine Imaam ni mwenye elimu lakini ana matatizo kutamka baadhi ya herufi sio kwa makusudi bali ndivyo alivyo. Hapo pia kutakuwa hakuna tatizo. Hivyo, ikiwa Sunnah ya kuchagua Imaam mwenye kisomo cha Qur-aan itafuatwa tatizo hilo halitokuwepo. Na pia ikiwa Imaam raatib (aliyeteuliwa wa kudumu) hayupo, Waumini wakawa ni wenye kuchaguana kwa sifa hiyo, tatizo hilo pia halitokuwepo. Tatizo ni kuwa kuna watu wenye kupenda kujitanguliza kuswalisha Imaam ikiwa hayupo pamoja na kuwa anajua hana sifa za Uimaam. Akiwa atafanya hivyo, yeye atakuwa na makosa na Maamuma hawatokuwa na dhambi. Lakini ni jukumu lao kutomkubalia Muislamu huyo kuswalisha kwa njia nzuri ya mazungumzo bila fujo maadam hana sifa zistahikizo. Na Allaah Anajua zaidi




Vitambulisho: