Dhahabu Zinatolewa Zakaah?

SWALI: Asalam alaykum. Je mwanamke mwenye mapambo ya dhahabu itabidi atolee zakah? Naomba nifafanulie vizuri

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Mtukufu, Swalah na salamu zimfikie kipenzi chetu, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Ahli zake na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na Watangu Wema na waliowafuata kwa kheri mpaka Siku ya Qiyaamah. Shukrani kwa swali lako ambalo mara nyingi huwa linakosewa kueleweka na wengi. Mapambo ya kuvaa na katika mas-ala ambayo Maulamaa wamekhtilafiana kama yanapasa kutolewa Zakaah au hayapasi kutolewa. Maulamaa wengine wamesema kuwa mapambo ni fardhi kutolea Zakaah kwa sababu yamo katika maana ya Aayah: ((Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu)). [At-Tawbah: 34] Na hakika kauli ya Jamhuur ni kuwa dhahabu ambazo zinatumika kama mapambo na zikafika Niswaab (kiwango cha chini ambacho mtu akiwa nacho anastahiki kutoa Zakaah baada ya kupita mwaka) itabidi aitolee Zakaah kutokana na dalili zifuatazo: Imesimuliwa kutoka kwa 'Amr bin Shu'ayb kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kwamba mwanamke alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa na mtoto wake wa kike ambaye alivaa bangili mbili nene za dhahabu. Akamwambia:"Je, umezitolea Zakaah hizo?" Akasema: "Hapana" Akasema: Je, utapenda Allaah Azibadilishe kuwa bangili mbili za moto siku ya Qiyaamah? "Akazivua na kumpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kusema "Hizi ni za Allaah na Mjumbe Wake")) [Abu Daawuud, An-Nasaaiy na ni Hadiyth Hasan] Imetoka kwa Ummu Salamah ambaye amesema: "Nilikuwa nikivaa mapambo ya dhahabu na nikasema: Ewe Mjumbe wa Allaah, hii ni kanz (hazina kama iliyokusudiwa katika Surah At-Tawbah 9: 34) Akasema: "Chochote kinachofikia kiasi ambacho Zakaah inapasa, basi lipia Zakaah, kisha hakitakuwa ni kanz". [Abu Daawuud, Ad-Daraaqutniy, Al-Haakim, Al-Bayhaaqiy] Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja kwangu siku moja na akaona nimevaa pete za fedha. Akasema: Nini hii ewe 'Aaishah? Nikasema: Nimezitengenezesha ili nijipambe kwa ajili yako ewe Mjumbe wa Allaah. Akasema: Je, unazilipa Zakaah? Nikasema: Hapana, au Alivyotaka Allaah (niseme). Akasema: Hiyo itatosheleza kukupeleka motoni" [Abu Daawuud, Ad-Daaraqutniy, Al-Haakim na Al-Bayhaaqiy] Na kiwango cha chini ni kuwa na dhahabu yenye uzani wa gramu 82.5. Hii ni kwa ile Hadiyth ya 'Amr bin Shu'ayb hapo juu. Na pia Hadiyth ya Asmaa bint Yaziyd na ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni ushahidi wa hayo. Kiwango cha kutoa ni asilimia 2.5 ya dhahabu uliyo nayo . Na Allaah Anajua zaidi
Vitambulisho: